Sheria na Mahakama

Yaliyojiri kesi ya Aveva na Kaburu leo

Tarehe October 4, 2017

Kesi ya utakatishaji fedha na kugushi nyaraka inayowakabili Rais wa Simba, Evans Aveva na Makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ imeahirishwa hadi Oktoba 11, 2017 kwa sababu upelelezi haujakamilika.

Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha Dola za Kimarekani 300,000.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi15, 2016 wakionesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa Dola za Kimarekani 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli.

Katika shtaka la pili inadaiwa kuwa Machi 15, 2016 katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe Ilala, Aveva alitoa nyaraka ya uongo ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15, 2016 wakati akijua ni uongo na kosa.

Katika shtaka la tatu la kutakatisha fedha, Aveva na Nyange wanadaiwa kuwa kati ya Machi 15 na Juni 29, 2016 Jijini Dar es Salaam,  kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata Dola za Kimarekani 300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.

Kwa upande wa shtaka la nne la kutakatisha fedha, Aveva anadaiwa kuwa Machi 15, 2016 katika benki ya Barclays Mikocheni alijipatia Dola za Kimarekani 300,000 wakati akijua zimetokana na kughushi.

Katika shtaka la tano la kutakatisha fedha, mshtakiwa Nyange anadaiwa kuwa Machi 15, 2016 katika benki ya Barclays tawi la Mikocheni alimsaidia Aveva kujipatia Dola za Kimarekani 300,000 wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.

Washtakiwa wote wapo rumande hadi sasa kwa sababu shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni