Sheria na Mahakama

Watatu kizimbani kwa mauaji ya mwanaharakati wa ujangili meno ya tembo

Tarehe October 10, 2017

Watu watatu wakiwemo ndugu wawili wamepandishwa kizimbani kwa mauaji ya mwanaharakati wa kupinga ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo, Wayne Lotter.

Watuhumiwa hao, Khalid Mwinyi na Rahma Mwinyi na Mohammed Maganga wamefikishwa katika Mahakamani ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es Salaam, na kusomewa mashtaka hayo ya mauaji mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Akiwasomea mashtaka hayo, Wakili wa Serikali, Adolf Mkini amedai kuwa watuhumiwa hao wanadaiwa Agosti 16 katika makutano ya barabara ya Chole na Haile Selasie Wilayani Kinondoni walimuua kwa kumpiga risasi Lotter aliyekuwa akifanya kazi na kampuni ya Pams Foundation ya Arusha.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri la mauaji isipokuwa Mahakama Kuu.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi wa kesi haujakamilika na kesi hiyo kuahirishwa hadi Oktoba 23,mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa kupelekwa rumande kwa sababu shtaka linalowakabili halina dhamana kisheria.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni