Sheria na Mahakama

Vigogo Tanesco wapandishwa kizimbani kwa hasara ya bilioni 2.7

Tarehe November 8, 2017

Maofisa wanne wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na watu wengine wawili wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 202 ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya bilioni 2.7.

Akiwasomea mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi aliyekuwa akisaidiana na wakili wa serikali Gloria Mwende amesema watuhumiwa wote wanakabiliwa na tuhuma za kula njama, kutoa taarifa za uongo, kuisababishia hasara serikali na mashtaka 199 ya wizi.

Imedaiwa kuwa, kati ya Januari 7, 2014 na Januari 31,2015 jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote hao walikula njama ya kutenda kosa la wizi.

Katika shtaka la pili, imedaiwa kuwa, tarehe hizo, katika ofisi ya Tanesco Kinondoni, iliyopo Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, washtakiwa, Mlowe,Ngella,  Maira na Jonas wakiwa ni waajiriwa wa Tanesco Kinondoni, wakiwa na uwezo wa kuingia katika mfumo wa kompyuta unaojulikana kama Tansms33, wakiwa na nia ya kulaghai walifanya maingizo ya uongo katika mfumo huo ya kiasi cha  Sh 2,746,485,545.63 wakijaribu kuonyesha kuwa fedha hizo zililipwa kwa Tanesco  na mawakala wa tatu (Luku Vendos) kama manunuzi ya umeme wa Luku (unit).

Katika shtaka la 202 washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kusababisha hasara ambapo wanadaiwa kuwa kati ya Julai Mosi ,2014 na Machi 31,2016 washtakiwa hao kwa matendo yao waliisababishia Tanesco kupata hasara ya Sh 2,746,485,545.63/-.

Washtakiwa hao hawakuruhusiwa kuongea kitu chochotemahakamani hapo kwa sababu Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi za uhujumu uchumi hadi Mahakama Kuu.

Kwa mujibu wa upande wa Mashtaka, upelelezi wa kesi huyo bado haujakamilika na washtakiwa wamerudishwa rumande hadi Novemba 2, mwaka huu.

Washtakiwa hao ni pamoja na, Afisa Mapato Mwandamizi, Emmilian Mlowe, Mhasibu wa Mapato msaidizi, Shakira Ngella,  meneja wa fedha mwandamizi Mkama Maira na Mhasibu wa udhibiti wa Mikopo Yaned Jonas.

Washtakiwa wengine ni, Bashiru Ngella na Barnabas Massaly.

Hakimu Nongwa amewashauri washtakiwa hao kuomba dhamana katika Mahakama Kuu kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Mafisadi.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni