Sheria na Mahakama

Vielelezo vya kesi ya Kitila na wenzake kutoka Uingereza vyapokelewa

Tarehe June 17, 2017

Harry Msamire Kitilya (kushoto) na Sioi Graham Solomon (kulia) wakiwa mahakamani.

Harry Msamire Kitilya (kushoto) na Sioi Graham Solomon (kulia) wakiwa mahakamani.

Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Kamishna Mkuu Mstaafu wa TRA, Harry Kitilya na wenzake umeieleza mahakama kuwa wamepokea awamu ya kwanza ya vielelezo kutoka nchini Uingereza.

Wakili wa Serikali, Christopher Msigwa amesema hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Msigwa ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wanatarajia awamu ya pili ya vielelezo kuwasili nchini Tanzania wakati wowote kuanzia sasa.

Hata hivyo wakili wa utetezi, Mwanahamisi Adam ameuomba upande wa mashtaka kueleza muda muafaka ambao utatumika kwa vielelezo hivyo kufika nchini.

Aidha Hakimu Mkeha amewaambia upande wa mashtaka huo muda wowote wanaoutaja wahakikishe unaangukia ndani ya siku 14 na ikishindikana basi Juni 30 mwaka huu waeleze vielelezo hivyo vitafika ndani ya siku ngapi.

Miezi miwili iliyopita upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa upelelezi dhidi ya kesi hiyo uliokuwa unafanywa ndani ya nchi umekamilika na kuwa bado wanasubiri upepelelezi unaofanywa nje ya nchi.

Mbali na Kitilya washtakiwa wengine ni Miss Tanzania, 1996, Shose Sinare na Sioi Graham Solomon.Wanadaiwa kutenda makosa nane likiwemo la utakatishaji wa fedha wa kiasi cha USD milioni sita.

Mbali na shtaka la utakatishaji wa fedha, watuhumiwa hao wanakabiliwa na tuhuma za kula njama, kutoa nyaraka za uongo na kughushi.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya Machi2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa Mkopo wa USD 550 wa Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard ya Uingereza.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni