Sheria na Mahakama

Shahidi adai Kanumba alikuwa na maumivu ya moyo na sumu mwilini

Tarehe October 25, 2017

Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam leo katika kesi ya mauaji ya bila kukusudia inayomkabili muigizaji wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’, imeelezwa kuwa Marehemu Kanumba alikuwa akifanya mazoezi ya kutanua misuli ambayo alishauriwa aachane nayo.

Maelezo hayo yamesomwa mahakamani na Askari wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Jijini Dar es Salaam, Sajenti Nyagea mbele ya Jaji Sam Rumanyika akisoma maelezo ya Josephine Mushumbusi ambayo aliyatoa polisi.

Mushumbusi ambaye pia ni mke wa Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema, Dkt. Wilbroad Slaa yupo nchini Canada kwa sasa.

Katika maelezo hayo, Mushumbusi ambaye ameeleza kuwa alikuwa na kituo cha tiba mbadala na alikuwa akimtibu Kanumba, amedai kuwa marehemu Kanumba alimueleza pia kuwa alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya moyo.

Ameeleza kuwa Kanumba alikuwa akisumbuliwa na matatizo mbalimbali na wakati akimhudumia alibaini kuwa alikuwa akifanya mazoezi ya kutanua misuli na kumshauri aachane nayo.

Maelezo hayo yameongeza kuwa siku Kanumba alipokwenda kwake alikuwa na watu wengi, hivyo alimuomba apange siku nyingine ambapo kabla ya kuonana alisikia kuwa amefariki dunia.

Akimnukuu Mushumbusi, askari huyo alisoma kama ifuatavyo;

“Nasema kwamba mimi ndio mwenye jina la Josephine S Mushumbusi, pia ni mmiliki wa kituo cha Tiba Mbadala cha Precious kilichopo maeneo ya Mawasiliano Tower (Sam Nujoma).

Nina wateja wengi wa umri tofauti, mmoja wa wateja wangu ni Steven Kanumba ambaye kwa sasa ni marehemu.

Nakumbuka August 2011 ndio nilimfahamu Kanumba ambapo alikuja akiwa na tatizo akitaka nimtoe sumu katika mwili wake.

Kuanzia hapo akawa anakuja katika kliniki yangu mara kwa mara kwa ajili ya huduma hiyo.

Kila alipokuja nilikuwa nampima kwa kutumia mashine ya kutolea sumu ambapo kwa kufanya hivyo niligundua ana mafuta (cholesterol) na tatizo la moyo.

Pia alikuwa na upungufu wa hewa katika ubongo wake ambapo hali hiyo ilimletea udhahifu katika mwili.

Mfano alikuwa na tatizo la maumivu ya moyo mara kwa mara, ubongo na akili ilichoka.

Katika kumuhudumia niligundua anafanya mazoezi ya kutanua misuli mara kwa mara ambapo nilimwambia aache kwa sababu mfumo wake wa damu sio mzuri, hivyo anaweza kusababisha kifo.

Kama kujua mtu kafa kwa kukosa hewa, misuli yake akifa inakuwa na rangi ya Blue.

Pia aliwahi kunambia ana matatizo makali ya moyo ila hakunambia yanasababishwa na nini, hivyo akaniomba ushauri nasaha.

Hivyo tulipanga appointment kwa ajili ya kumpa ushauri nasaha ila siku chache baadae nikasikia amefariki dunia.”

Baada ya kusoma maelezo hayo, Staff Sajenti, E 103 Nyangea (53) aliiomba mahakama iyapokee kama kielelezo ambapo mahakama ilikubali.

Hata hivyo, upande wa mashtaka kupitia Wakili wa Serikali, Faraja George uliiomba mahakama imtambue askari huyo kama shahidi na sio msomaji wa maelezo ya Mushumbusi.

Kutokana na mvutano wa kisheria, Jaji Rumanyika alitoa uamuzi kuwa askari huyo atatambulika kama shahidi.

Kwa maelezo ya Mushumbusi, upande wa utetezi umefunga ushahidi wake na kesho Oktoba 26, 2017, wazee wa baraza watatoa maoni yao kabla ya mahakama kutoa hukumu yake.

Lulu ambaye yupo nje kwa dhamana anakabiliwa na kesi ya mauaji ya bila kukusudia ya msanii wa filamu, Steven Kanumba, akidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 7, 2012 nyumbani kwa marehemu, Sinza Vatican, Jijini Dar es Salaam.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni