Sheria na Mahakama

Mwalimu Madrasa atupwa jela miaka 30 kwa kulawiti

Tarehe October 3, 2017

Mwalimu wa Madrasa, Mkazi wa Gongo la Mboto, Abdillah Sharifu (30), leo amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kumlawiti mtoto wa kiume wa miaka 11.

Mshtakiwa huyo aliyehukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Ilala, anadaiwa kumlawiti mtoto huyo na kumtishia kumloga endapo angetoa taarifa kwa wazazi wake juu ya unyama huo.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassan, amesema ameridhishwa na ushahidi wa mashahidi wanne akiwemo daktari na kumtia hatiani mshtakiwa.

“Mshtakiwa nimekutia hatiani kama ulivyoshtakiwa, ninakuhukumu kifungo cha miaka 30 jela kwa kitendo hiki cha kikatili ili iwe fundisho kwako na watu wengine wenye tabia mbaya kama hii,” amesema Hakimu Hassan kwa mshtakiwa ambaye ni mwalimu wa dini.

Hakimu Hassan amesema shahidi wa kwanza ambaye ni mtoto husika aliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa  ambaye ana mke mwenye tatizo la kuona, Februari 25 alimtaka mtoto huyo kwenda nyumbani kwake na baada ya kufika alimuamuru kuvua nguo kitendo ambacho pia kilifanywa na Sharifu.

Shahidi huyo amedai kuwa mshtakiwa alimfanyia ukatili huo, huku akimtishia kuwa iwapo angethubutu kutoa siri hiyo angemloga.

“Mara kwa mara alikuwa akinifanyia mchezo huu hadi nilipomwambia mama na kisha kwenda kufungua kesi katika kituo cha polisi Mazizini,” alisema mtoto huyo katika ushahidi alioutoa mahakamani.

Katika ushahidi wa mama mzazi wa mtoto huyo, alidai baada ya kuripoti polisi walikwenda hospitali ambako kwa mujibu wa vipimo vya daktari licha ya kutokuwa na michubuko ilionekana aliingiliwa.

Mshtakiwa alidai ana mke kipofu na kwamba, hafanyi vitendo hivyo isipokuwa alikuwa na ugomvi na mama wa mtoto huyo na ndiyo sababu ya kumfungulia kesi.

Hata hivyo, mshtakiwa alishindwa kuifafanulia Mahakama chanzo cha ugomvi hivyo ilitupilia mbali utetezi wake na kumtia hatiani.

Awali, Wakili wa Serikali, Grace Mwanga aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia za kulawiti watoto na wanaotumia kimvuli cha nyumba za ibada kufanya ukatili.

Mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo, Februari 25 katika eneo la Moshi Baa, Gongo la Mboto, Jijini Dar es Salaam.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni