Sheria na Mahakama

Mahakama Kuu Gambia kusikiliza ombi la Jammeh kubatilisha matokeo

Tarehe January 10, 2017

Yahya Jammeh, amekuwa Rais wa Gambia kwa miaka 22

Yahya Jammeh, amekuwa Rais wa Gambia kwa miaka 22

Mahakama Kuu nchini Gambia leo inatarajia kusikiliza ombi la Rais Yahya Jammeh dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika mwezi Desemba, mwaka jana.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, matokeo ya uchaguzi huo yalimpa ushindi Adama Barrow kwa asilimia 43 ya kura.

Lakini Jammeh anataka mahakama ipitishe kwamba Adama Barrow hakuchaguliwa kutokana na mapungufu yaliyokuwepo wakati wa upigaji kura.

Tayari inasemekana kuwa baadhi ya mahakimu wa mahakama kuu hawatakuwepo huku Waziri wa Habari wa Gambia akidaiwa kuondoka nchini humo.

Yahya Jammeh ambae mwanzoni alikubali kushindwa katika uchaguzi wa urais wa mwezi jana, ghafla alibadili msimamo na kutaka uchaguzi huo ubatilishwe, kwa madai kuwa kuna makosa yaliyofanywa na tume ya uchaguzi.

Wakati huo huo, Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi ECOWAS inajaribu kutafuta suluhu ya kidiplomasia ili kuepusha vurugu na machafuko ambayo yanaweza kuenea nchi nzima.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, ambae ametajwa kama ndio msuluhishi, ataelekea Banjul kesho na Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia pamoja na aliyekuwa rais wa Ghana John Dramani Mahama.

Hii inaweza kuwa ndio safari ya mwisho ya kujaribu kumshawishi Jammeh kuachia madaraka na kumpisha rais mteule Adama Barrow.

Sherehe za kuapishwa kwa rais mpya zimepangwa kufanyika siku ya Alhamisi, tarehe 19 mwezi huu.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni