Sheria na Mahakama

Apandishwa kizimbani kwa kuandika uongo mazungumzo Acacia na Serikali

Tarehe October 4, 2017

Mkazi wa Chato Mkoani Geita, Obadia Frank (41), amefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu tuhuma za kuchapisha taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook kuhusu mazungumzo kati ya Serikali na wawakilishi wa kampuni ya Acacia.

Akisoma mashtaka dhidi ya mshtakiwa huyo mbele ya Hakimu Mkazi, Wilbard Mashauri, Wakili wa Serikali, Leonard Challo, amedai kuwa mshtakiwa huyo ambaye ni wakala wa Bayport alitenda kosa hilo Agosti 8 mwaka huu, katika Wilaya ya Chato Mkoani Geita kwa kuchapisha taarifa kupitia ukurasa wake wa Facebook iliyokuwa ikihusiana na mazungumzo kati ya serikali na kampuni ya Acacia.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kusambaza maneno kuwa “Taarifa kutoka kikao cha mazungumzo kati ya Serikali na wawakilishi wa kampuni ya Acacia kuwa wanasheria wa upande wetu wanashindwa kutafsiri baadhi ya vifungu vya sheria hadi kufikia kuomba msaada kwa wanasheria wa Acacia sasa huoni hivi ni vituko mwizi anakusaidia sheria haahaa haha.”

Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo aliendelea kusambaza maneno kuwa, “mazungumzo bado yanaendelea lakini wanasheria wetu wamebanwa sana ukizingatia wale jamaa wana vielelezo vyote vya mikataba kiukweli tumuombe Mungu maana Serikali ikitaka kuvunja mkataba na Acacia gharama kubwa zitatuusu.”

Kwa mujibu wa Wakili huyo wa Serikali, maneno hayo yalikuwa na lengo la kupotosha umma.

Hatahivyo, mshtakiwa huyo alikana shtaka hilo na kesi hiyo kuahirishwa hadi Oktoba 16, mwaka huu na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana baada ya kukaa Polisi siku 43.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni