Michezo/Sports

TFF yamjibu Zitto kususia mechi dhidi ya Libya

Tarehe December 1, 2017

Zitto Kabwe. 

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema kuwa suala lililoibuliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ni nyeti sana na kwamba uongozi wa juu wa TFF utalitolea majibu hivi karibuni.

Afisa Habari wa TFF, Alfred Lucas amesema hayo leo ikiwa ni majibu ya hoja ya Zitto ya kuitaka Tanzania isusie kucheza mechi dhidi ya Libya ili kupinga vitendo vya biashara ya utumwa inayoendelea nchini humo.

“Msimamo utatolewa na viongozi wangu mara baada ya kukaa na kutafakari hali halisi kwa sasa, na wenye uwezo wa kukaa na kutafakari ni viongozi wa juu, itakapokuwa tayari mtajulishwa,” amesema Lucas.

Jana, kupitia mitandao ya kijamii, Zitto alitoa wito kwa TFF kuitaka timu ya Kilimanjaro Stars isusie mechi inayotarajiwa kuchezwa dhidi ya Libya siku ya Jumapili katika michuano ya CECAFA kwa lengo la kuonesha kuchukizwa na vitendo vya biashara ya utumwa vinavyodaiwa kuendelea nchini humo.

Katika siku za hivi karibuni, Libya imegonga vichwa vya vyombo vya habari kwa tuhuma za kufanya biashara ya utumwa kwa kuwauza watu wenye asili ya Afrika (wahamiaji kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara) na kupelekea taasisi, mashirika, watu maarufu kujitokeza na kukemea kitendo hicho huku Serikali ya Libya ikituhumiwa kufumbia macho.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kuuzwa kwa thamani ya kati ya Dola za Marekani 200 hadi 300.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni