Makala Maalumu

Rais Donald Trump asiye na bahati Kombe la Dunia

Tarehe October 11, 2017

Wachezaji wa Trinidad & Tobago wakifurahia ushindi dhidi ya Marekani katika mtanange wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2018 nchini Russia.

Marekani iliyo mikononi mwa Rais Donald Trump imeshindwa kufuzu kucheza Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1990 nchini Italia. Imekuwaje?

Taifa hilo kubwa duniani kwa kila kitu limeshindwa baada ya kutandikwa kwa mabao 2-1 na Trinidad & Tobago katika mchezo ambao uliamua nafasi yake kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Russia.

Nafasi hiyo ilikuwa ni muhimu kwa taifa hilo lakini haikuwa hivyo na badala yake Panama ikapata nafasi baada ya kuigaragaza Costa Rica kwa mabao 2-1 huku Mexico ikizabuliwa na Honduras kwa mabao 3-2.

Ingekuwa kwenye mataifa yetu yanayoendelea tungekuwa na fikra Trinidad & Tobago mbona haifuzu inakwenda wapi, inapambana vipi si ingeachia Marekani ipite kirahisi?

Kumbe kila taifa linatafuta kutambulika duniani. Panama hawatakisahau kizazi chao kilichowafanya wasonge mbele kwa mara ya kwanza katika Kombe la Dunia.

Pia kumbukumbu hizo watazirudisha kwa kizazi cha Trinidad  &Tobago kwa kikosi kilichowasimamisha Marekani licha ya jina lao kuwa ni dogo katika ulimwengu wa soka.

Rais wa 45 wa Marekani Donald Trump

Rais wa Panama Juan Carlos Varela Rodriguez ametangaza siku ya mapumziko kwa taifa lake kwa kupata nafasi hiyo adimu kwenda Kombe la Dunia.

Hata ingekuwa kwetu huku Tanzania nasi nahisi tungefanya hivyo kwani ni nafasi inayowaniwa na mataifa mengi na kwa hisia tofauti. Kuna siku Tanzania nayo itakuwa kama Panama.

Tuachane na Panama, turudi nchini Marekani. Trump anakuwa Rais wa Kwanza wa Marekani kwa miaka 27 kushuhudia taifa hilo likishindwa kwenda katika fainali za Kombe la Dunia.

Enzi za Utawala wa George H. Bush ambaye alikuwa Rais wa Marekani wa 41 taifa hilo lilifuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Italia. Fainali hizo zilianza Juni 8 na kumalizika Julai 8.

Costa Rica na Marekani zilifuzu kutoka ukanda wa CONCACAF. Marekani ilipangwa kundi A na wenyeji Italia, Czechoslovakia na Austria. Marekani ilirudi bila pointi jijini Washington baada ya kuzabuliwa michezo yote. Wakati ikifuzu wakati huo barani Afrika Misri na Cameroon ndizo zilifika fainali hizo. Misri nayo tangu wakati huo ndio imefuzu tena fainali za Russia baada ya miaka 27.

Baada ya kutoka Rais George H. Bush kijiti ca kuliongoza taifa hilo akachukua Bill Clinton ambaye alikuwa na bahati ya kushuhudia taifa hilo likienda Kombe la Dunia mara mbili mwaka 1994 Marekani ilipokuwa wenyeji na 1998 nchini Ufaransa. Nchini Ufaransa kutoka ukanda wa CONCACAF Marekani ilifuzu pamoja na Jamaica na Mexico.

Christian Pulisic katika mchezo dhidi ya Trinidad & Tobago

Rais wa 43 wa Marekani George W. Bush licha ya mambo yote alikuwa na furaha pale aliposhuhudia taifa lake likienda Kombe la Dunia mara mbili mwaka 2002 nchini Korea Kusini na Japan pia nchini Ujerumani mwaka 2006.

Barack Obama akachukua mikoba ya Rais Bush ya kuongoza taifa hilo ambaye naye alishuhudia Marekani ikienda Afrika Kusini mwaka 2010 katika fainali za Kombe la Dunia lililofanyika kwa mara ya kwanza katika ardhi ya Afrika.

Marekani ilifuzu kutoka CONCACAF na Costa Rica, Mexico, na Trinidad & Tobago. Pia mwaka 2014 nchini Brazil Obama alishuhudia taifa lake likizama kwa wakali wa soka. Obama alimkabidhi Trump kijiti Januari 20, 2017 cha kuongoza taifa hilo lakini ameanza kwa bahati mbaya ikiwa ni miezi 10 tangu ashike wadhifa huo. Panapo majaliwa huenda Mwenyezi Mungu akamjalia mwaka 2022 akashuhudia taifa lake likienda Qatar kwa ajili ya fainali hizo.

Pulisic akitokwa na machozi akishindwa kuamini kilichotokea baada ya mchezo dhidi ya Trinidad & Tobago.

Imetayarishwa na Jabir Johnson.

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni