Makala Maalumu

Ndoto za Urais za George Weah zatimia

Tarehe October 12, 2017

UNAPOLITAMKA jina la George Oppong Weah, basi linakuwa na maana sana katika ardhi ya Afrika hususani mashabiki wa kandanda ambao ni yeye tu hadi sasa makala hii inapoandikwa kutoka katika ardhi yenye nchi 54 kutwaa Tuzo ya Mchezo Bora wa Dunia ambayo kwa sasa imeshikiliwa kwa muda mrefu na wachezaji wawili Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Imekuwaje hadi leo tunataka kujua historia yake ya kandanda na maisha yake ya kila siku? Ni sababu moja tu. Sasa anaweza kuwa Rais wa Taifa la Liberia. Hiyo ni kwasababu ya kinachoendelea nchini humo hadi leo.

Oktoba 10 mwaka huu wananchi wa Liberia walifanya uchaguzi mkuu nchini humo wa kumchagua Rais wa taifa hilo na taarifa za awali hadi sasa zinaonyesha kuwa Weah aliyetwaa Ballon d’or mwaka 1995 anaongoza dhidi ya mpinzani wake ambaye ni makamu wa Rais wa taifa hilo Joseph Boakai

Licha ya dosari za hapa na pale Tume ya uchaguzi nchini humo inatarajiwa kutangaza mrithi wa Rais Ellen Johnson Sirleaf.

George Weah akiwa na tuzo ya Balon d’Or mwaka 1995.

Sirleaf ni rais wa kwanza mwanamke barani Afrika ambaye alishinda uchaguzi wa 2005 kufuatia kipindi cha mpito baada ya vita na baadaye alishinda tena 2011.

Wapigakura milioni 2.1 walioandikishwa walipiga kura zao kumchagua rais kutoka idadi ya wagombea 20, ikiwa ni pamoja na mwanamke mmoja na kuwachagua wabunge 73 wa baraza la wawakilishi.

Iwapo kati ya wagombea hao hakuna atakayefikisha asilimia 50 wagombea wawili waliopata idadi kubwa watachuana tena kwenye duru ya pili itafanyika Novemba 7. Wachambuzi wa mambo wameashiria uwezekano wa uchaguzi huo kwenda duru ya pili.

HISTORIA YA GEORGE WEAH

Baada ya kuisha kwa vita vya pili vya ndani ya Liberia Weah akatangaza nia yake ya kuwania uraisi wa nchi yao katika uchaguzi wa mwaka 2005 akiunganisha chama cha Congress for democratic Change.

Pamoja na kuwa maarufu zaidi nchini Liberia, upinzani ulitumia kampeni zake kumkosoa kwa kukosa elimu ya darasani kama kikwazo cha yeye kuiongoza nchi ukilinganisha na mpinzani wake Ellen Johnson Sirleaf ambae alisoma katika chuo cha Harvard.

Wachambuzi pia wa masuala ya kisiasa nchini Liberia walimzungumzia Weah kama mwanasiasa asiye na uzoefu, huku mama Ellen akiwahi kuwa waziri wa fedha kuanzia miaka ya 1970 huku akifanya kazi katika benk ya dunia.

Weah pia alizua maswali kutokana na awali kupewa uraia wa Ufaransa akiwa Paris Saint Germain (PSG) kama mchezaji. Mahakama ilimuondolea vikwazo hivyo vyote na kumruhusu agombee.

Alitikisa nchi nzima kutokana na umaarufu wake lakini matokeo ya mwisho ya uchaguzi yalimpa ushindi mama Ellen Sirleaf kwa ushindi wa 59.4% dhidi ya 40.6% alizopata Weah.

Matokeo hayo ya uchaguzi yalisababisha vurugu kutoka kwa wafuasi wa Weah ambao hawakuridhishwa na taratibu za uchaguzi pamoja na matokeo.

Lakini baadae wadau wa masuala ya siasa nchini Liberia waliwaomba wafuasi wa Weah wakubali matokeo kwani uchaguzi ulikua halali. Kasha bibi Ellen akatangazwa raisi nchini Liberia. Suala la elimu lilikua ni tata nchini Liberia kutoka kwa upinzani na hata kumfanya ashindwe tena kumzuia bibi Ellen Sirleaf katika uchaguzi wa mwaka 2011. Weah akachaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa chama cha Congress for Democratic Change.

Weah alizaliwa Oktoba Mosi, 1966 huko Grand Kru, Liberia. Alitangazwa mchezaji bora wa dunia mwaka 1995, huku akishinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika mara tatu. Mwaka 2004 aliandikwa katika orodha ya wachezaji 100 bora wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ambao bado wanaishi.

George Weah alitua barani Ulaya mwaka 1988 baada ya kusajiliwa na kocha Arsene Wenger, akiifundisha AS Monaco kipindi hicho. “Weah ni kipaji cha ajabu. Sijawahi ona mchezaji akijituma kama yeye uwanjani” alikaririwa kocha wa sasa wa Arsenal ya Uingereza, Wenger

Mwaka 1991 Weah alikua katika kikosi cha Monaco kilichoshinda Kikombe cha Ligi ya Ufaransa. Alijiunga na Paris Saint Germain (1992-1995) akishinda kikombe cha ligi mwaka 1994 na kuwa mfungaji bora wa klabu bingwa Ulaya msimu huo huo wa 1994-1995 akifunga magoli 16 katika mechi 25 alizocheza za Ulaya huku akifunga goli la kustaajabisha dhidi ya Bayern Munich katika michuano hiyo mikubwa barani Ulaya.

Weah alijiunga na AC Milan mwaka 1995 na kushinda kikombe cha ligi ya Italia 1996 na 1999. Mwaka 1995 alishinda tuzo ya Ballon d’Or na kutangazwa mchezaji bora wa FIFA. Weah akawa mchezaji maarufu zaidi katika kikosi cha Milan baada ya kufunga goli la uwezo binafsi, ‘solo goal’ dhidi ya Verona katika dimba la San Siro akiwapiga chenga wachezaji saba kabla ya kufunga.

Baada ya kuondoka Milan Januari 2000, Weah alijiunga Chesea, Manchester City na Olympique Marseille kwa mafanikio ya haraka, kabla ya kuondoka Marseille mwezi Mei 2001 akielekea Al Jazira FC ya Falme za Kiarabu, ambako alicheza na kustaafu soka lake mwaka 2003.

Pamoja na mafanikio makubwa katika ngazi ya klabu, Weah alishindwa kufanya hayo akiwa na timu ya taifa ya Liberia. Alifanya kila alichoweza katika timu ya taifa katika kucheza, kufundisha na kuiwezesha kifedha lakini akishindwa kuisaidia kufuzu hata mara moja katika fainali za kombe la dunia. Huku wakishindwa kwa pointi moja tu kufuzu katika fainali za kombe la dunia zilizo fanyika 2002.

Weah aliichezea Liberia michezo 60 katika kipindi cha miaka 20 na kufunga magoli 22. Amekua ni mchezaji muhimu wa Liberia huku akiwa kocha kipindi fulani na kuwawezesha kifedha.

Imetayarishwa na Jabir Johnson

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni