Makala Maalumu

Majonzi yatawala Italia

Tarehe November 14, 2017

Matukio baada ya mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2018 baina ya Italia na Sweden.

Haitasahaulika Novemba 13, 2017 katika soka la Italia pale timu ya taifa hilo maarufu Azzuri iliposhindwa kufuzu kucheza Kombe la Dunia 2018 litakalofanyika nchini Russia.

Tukio hilo limetokea ikiwa ni miaka 60 ya kuwamo kwenye kila fainali ya Kombe la Dunia. Mabingwa hao mara nne wa taji hilo wakicheza na Sweden katika mchezo ambao uliipeleka Sweden Kombe la Dunia walitoka sare tasa ikiwa ni uwiano wa bao 1-0.

Mlinda mlango ambaye anashikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi katika timu ya taifa hilo Gianluiggi Buffon alibubujikwa na machozi pale aliposhuhudia kikosi cha miamba hiyo chenye wapenzi na mashabiki wengi ulimwenguni kikishindwa kutinga kwenye fainali hizo.

Italia ilishindwa kufuzu Kombe la Dunia kwa mara ya mwisho mwaka 1958. Wakati ule dunia nzima ilikuwa ikimzungumzia Mbrazil Pele lakini fainali za mwaka 2018 Neymar ndiye nyota wa Brazil aliye midomoni mwa wapenzi na  mashabiki wengi.

HISTORIA YA TIMU YA TAIFA YA ITALIA

Nazionale di Calcio Italiana kama ambavyo Waitaliano wenyewe wanavyopenda kuiita Timu ya Taifa ya Italia ipo chini ya Shirikisho la Soka la Italia (FIGC).

Ni miongoni mwa timu zenye mafanikio makubwa ya soka hususani katika Kombe la Dunia  ikitwaa mwaka 1934, 1938, 1982 na 2006 pia ni timu iliyofika kwenye fainali mara mbili mwaka 1970 na 1994. Mwaka 1990 ilishika nafasi ya tatu katika Kombe la Dunia.

Mwaka 1978 ilisalia kushika nafasi ya nne. Mwaka 1934 ilikuwa ni timu ya kwanza kulitetea taji lake. Mwaka 1968 Italia ilitwaa taji la Ulaya ambalo kwa sasa linafahamika kwa jina la Euro.

Pia ilifika fainali mbili Euro 2000 na Euro 2012. Italia ina taji moja la Olimpiki ililotwaa mwaka 1936. Mafanikio makubwa katika Kombe la Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ilikuwa ni nafasi ya tatu mwaka 2013. Italia inayofahamika kwa Gli Azzuri inatumia uwanja wa mazoezi wa Coverciano, Florence yalipo makao makuu ya FIGC.

ITALIA KATIKA KIPINDI CHA 1946-1966

Mwaka 1949 wachezaji 10 kati 11 waliuawa  katika shambulio la anga (Superga Air Disaster) lililotokea Torino ambayo ilikuwa imetwaa mataji matano ya Serie A hivyo Italia haikufanikiwa kufuzu kucheza mzunguko wa pili wa kuwania kucheza Kombe la Dunia la 1950.

Hiyo ilitokana na kudhoofishwa na shambulio hilo. Baada ya hapo timu ikawa inasafiri kwa kutumia boti badala ya ndege ikihofia tukio jingine la anga. Katika kufuzu kucheza Kombe la Dunia mwaka 1954 na 1962 Azzuri iliishia mzunguko wa kwanza  na haikufuzu kabisa kucheza mwaka 1958.

Italia  haikufanikiwa kuingia katika michuano ya kwanza ya Ulaya mwaka 1960 kwa wakati huo ikiitwa European Nations Cup. Pia katika Euro 1964 iliishia kutolewa katika hatua ya 16 na USSR. Katika kushiriki Kombe la Dunia mwaka 1966 iliishia kuzabuliwa na Korea Kaskazini kwa bao 1-0 licha ya kupewa nafasi.

Kikosi cha Italia kilikuwa na wakali Gianni Rivera na Giacomo Bulgarelli ambao walishindwa kuivusha mzunguko wa kwanza dhidi ya Korea Kaskazini ambao hawakuwa na kiwango cha kuizidi Azzuri. Italia ililaumiwa sana iliporudi katika ardhi ya nyumbani huku mfungaji wa Korea Kaskazini Pak Doo-ik akishangilia kama Daudi kumuuwa Goliathi.

ITALIA YA 1988-2000

Mwaka 1986 aliondoka Kocha Bearzot kisha nafasi yake ikachukuliwa na Azeglio Vicini. Kocha huyo mpya alitoa nafasi kwa vijana chipukizi Ciro Ferrara na Gianluca Vialli.

Vialli ambaye alikuwa mshambuliaji wa Sampdoria wakati huo alifunga mabao yaliyoipa Italia kufuzu Euro 1988. Alionyesha kuwa ataimudu vema nafasi iliyoachwa na Altobelli ambaye alikuwa na mfanano katika ufungaji wa mabao yake.

Washambuliaji hao wawili waliimaliza Ujerumani licha ya Azzuri kutandikwa na USSR katika nusu fainali. Mwaka 1990 Italia walipata uenyeji wa kuandaa Kombe la Dunia kwa mara ya pili. Wakati huo Azzuri ilikuwa na vipaji katika ushambuliaji Salvatore Schillaci na chipukizi Roberto Baggio.

Licha ya kuwa na majina hayo katika ushindi wao katika mechi zote walizocheza Rome hawakuruhusu kutanguliwa bao katika mechi tano za kwanza wakiishia kupoteza katika nusu fainali wakitandikwa na mabingwa Argentina mjini Naples kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-3 baada ya kuwa sare 1-1 hadi muda wa ziada (a.e.t). Schilaci aliipa uongozi katika kipindi cha kwanza na Claudio Canniggia akaisawazishia Argentina kipindi cha pili.

Aldo Serena alikosa mkwaju wa penalti na mkwaju wa Roberto Bonadoni ukiokolewa na mlinda mlango wa Argentina Sergio Goycochea. Hata hivyo Azzuri ilijitahidi na kuizabua England kwa mabao 2-1 ambayo iliwapa nafasi ya tatu mjini Bari. Schillaci alifunga mabao sita katika michuano hiyo na kuwa mfungaji bora. Haikuishia hapo Italia ilishindwa kufuzu kucheza Euro 1992.

Katika Kombe la Dunia mwaka 1994 Italia ilipoteza katika mechi ya ufunguzi ikizabuliwa kwa bao 1-0 na Ireland kwenye dimba la Giants karibu na jiji la New York. Ikaja kushinda kwa 1-0 dhidi ya Norway jijini New York kisha sare ya 1-1 na Mexico kwenye dimba la RFK jijini Washington.

Ilifanikiwa kuvuka kundi E kwa uwiano wa mabao kutokana na timu zote kuwa sawa kwa pointi. Katika hatua ya 16 Italia ilipata ushindi wa mabao 2-1 na Nigeria kwenye dimba la Foxboro karibu na Boston, Baggio akisawazisha na kuongeza moja kwa mkwaju wa penalti katika a.e.t Baggio tena akarudi nyavuni katika robo fainali dhidi ya Hispania mjini Boston kwenye ushindi 2-1.

Mabao mengine mawili Baggio aliyafunga dhidi ya Bulgaria kwenye nusu fainali jijini New York kwenye ushindi wa mabao 2-1. Fainali ilichezwa jijini Los Angeles katika dimba Rose Bowl ambako walifika hatua ya changamoto ya mikwaju ya penalti  ambako walishindwa mbele ya Brazil kwa mikwaju 3-2 huku Baggio akiwa katika dozi ya sindano ya kuzuia maumivu baada ya kupata majeruhi ya nyama za paja kukosa mkwaju wa penalti uliogonga mtambaa panya.

Azzuri ilishindwa kuvuka hatua ya makundi ya Euro 1996. Iliwazabua Russia kwa mabao 2-1 lakini ikapoteza dhidi ya Jamhuri ya Czech kwa matokeo hayo hayo.. Gianfranco Zola alishindwa kuiokoa Italia dhidi ya Ujerumani kwa mkwaju wa penalti hivyo kutoka sare tasa.

Katika kampeni za Kombe la Dunia 1998 Azzuri walitandika England mjini London kwa mara ya pili, huku Zola akifunga bao pekee. Katika fainali za Kombe la Dunia ikairudia tena Italia kuamua nani wa kutwaa taji hilo kwa mikwaju ya penalti ikiwa ni mara ya tatu mfululizo. Kama ilivyokuwa kwa Mazzola na Rivera mwaka 1970 ndivyo ilivyokuwa Alessandro Del Piero na Baggio wakifanya kile kinachoitwa staffeta wakajikuta wakipoteza kwa mikwaju 4-3 baada ya sare tasa a.e.t

Katika michuano hiyo Baggio alifunga mabao mawili hivyo kusalia kuwa mchezaji wa Italia aliyefunga kwenye matoleo matatu tofauti ya Kombe la Dunia. Euro ya mwaka 2000 ilimuibua Francesco Totti. Neema ilikuwa upande wa Italia baada ya kuwatandika wenyeji Uholanzi katika nusu fainali.

Mlinda mlango Francesco Toldo aliokoa mkwaju wa penalti. Totti alijulikana kwa mkwaju wake wa penalti wa staili ya ‘cucchiajo’ yaani kijiko kwa waswahili inafahamika kama ‘kuchopu’. Katika fainali hizo Italia ilimaliza nafasi ya pili baada ya kupoteza dhidi ya Ufaransa kwa mabap 2-1 huku bao la dhahabu  likiwaokoa Les Bleus waliosawazisha sekunde 30 kabla ya muda wa majeruhi dakika ya 93. Baada ya kichapo hicho kocha Dino Zoff aliachia ngazi baada ya kupingwa kwa maneno makali na Rais wa AC Milan wakati huo Silvio Berlusconi.

Wachezaji wa kikosi cha timu ya taifa ya Italia wakiwa katika masikitiko baada ya kushindwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia.

ZAMA ZA GIAN PIERO VENTURA

Kocha Gian Piero Ventura alipokea mikoba ya Antonio Conte Julai 18, 2016 kwa mkataba wa miaka miwili. Mechi yake ya kwanza ilikuwa ya kirafiki dhidi ya Ufaransa katika dimba la San Nicola Septemba 1 wakiishia kutandikwa bao 3-1.

Siku nne baadaye alishinda mchezo wake wa kwanza dhidi ya Israel ukiwa ni wa ufunguzi wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia mjini Haifa, Israel kwa ushindi wa mabao 3-1. Italia ilimaliza nafasi ya pili ya kundi G nyuma ya Hispania hivyo kutakiwa kucheza mtoano na Sweden.

Katika mchezo huo ndio umeweka rekodi ya kwanza baada ya miaka 59 huku Giorgio Chiellini, Andrea Barzagli, Daniele De Rossi na nahodha Gianluigi Buffon wakitangaza kustaafu majukumu ya timu ya taifa.

Imetayarishwa na Jabir Johnson

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni