Makala Maalumu

Hizi zitavunjwa Oktoba 28?

Tarehe October 25, 2017

Oktoba 28 mwaka huu itakuwa siku nyingine muhimu katika kandanda baina ya miamba mikongwe Young Africans na Simba SC itakapokusanya mashabiki wa mchezo huo katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo kucheza Simba au Yanga ni fahari kwa mchezaji wa Tanzania. Lakini ni fahari zaidi iwapo atakuwa mchezaji ambaye atashiriki mechi baina ya timu hizo.

Inakuwa fahari zaidi iwapo mchezaji atafunga bao au mabao katika mechi ya watani wa jadi, kwani huwafanya maelfu ya mashabiki wa timu yake walitaje jina lake na kushangilia kwa raha zao. Wengine, hupewa zawadi kutokana na kufunga kwenye mechi hizo za watani.

Wapo waliolewa sifa na kupotea kwenye ramani ya soka haraka, kwa sababu tu ya kuvimba kichwa baada ya kufunga mabao mfululizo kwenye mechi za watani.

Said Sued ‘Scud’, alifunga bao pekee la ushindi kwenye mechi ya watani wa jadi, akiwa anaichezea Yanga alitikisa nyavu za Simba dakika ya saba katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara wakati huo, sasa Ligi Kuu Mei 18, mwaka 1991.

Huo ukiwa msimu wake wa kwanza kwenye klabu hiyo, hakika ilikuwa furaha kubwa kwake, kwani tangu hapo aliaminika na kuwa mchezaji wa kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga.

Chipukizi huyo wa wakati huo, alipata ngekewa ya kuifunga tena Simba katika mchezo uliofuata wa marudiano wa ligi baina ya watani wa jadi, likiwa pia bao pekee la ushindi Agosti 31, mwaka huo huo 1991, jambo ambalo lilimfanya awe maarufu zaidi.

Cha kustaajabisha, Scud hakurejea kwenye kikosi cha Yanga cha mwaka 2002 na huo ukawa mwisho wa umaarufu wake kwenye soka ya Tanzania.

Kama wapo wanaodhani Scud alifanya kubwa sana katika historia ya watani wa jadi, watakuwa wapo mbali kabisa na ukweli, kwani Abdallah Kibadeni maarufu kama Chifu Mputa ama King, au Ndululu kama walivyokuwa wakimuita Wakenya, anaweza kusimama na kusema ana kubwa la kujivunia katika historia ya mechi baina ya Simba na Yanga ambapo sasa Kibadeni ndiye mchezaji pekee hadi sasa aliyeweza kufunga mabao matatu (hat trick) peke yake katika mchezo mmoja kwenye mechi za watani wa jadi katika Ligi.

Hiyo ilikuwa ni Julai 19, 1977 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, sasa Uwanja wa Uhuru, wakati Yanga ilipotandikwa 6-0 na Simba.

Siku hiyo, Kibadeni alitikisa nyavu za Yanga katika dakika za 10, 42 na 89, wakati mabao mengine ya Wekundu wa Msimbazi, yalitiwa kimiani na Jumanne Hassan ‘Masimenti’ dakika ya 60 na 73 na jingine Selemani Sanga wa Yanga alijifunga mwenyewe dakika ya 20 katika harakati za kuokoa krosi ya Ezekiel Greyson ‘Jujuman’.

Hivyo siku hiyo mbali na Simba kushangilia kulipa kisasi cha kulala 5-0 kwa Yanga, Juni Mosi mwaka 1968, Kibadeni alikuwa ana sherehe binafsi za kutumbukiza mabao matatu peke yake kwenye mechi baina ya watani hao, jambo ambalo liliwashinda wengi kabla yake kati ya waliowahi kuvaa jezi za Simba au Yanga.

Hakuna cha Sunday Manara ‘Computer’ wala Maulid Dilunga ‘Mexico’ aliyewahi kufanya hivyo zaidi ya King Kibadeni pekee.

Je, Oktoba 28, 2017 itaweza kuwekwa kwenye rekodi za watani? Ibrahim Ajibu, Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi, Shizza Kichuya, Donald Ngoma wanaweza kuandika upya historia?

Imetayarishwa na Jabir Johnson.

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni