Michezo/Sports

Chadema yajitoa timu ya bunge

Tarehe December 8, 2017

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wachezaji wa timu ya Bunge la Burundi muda mfupi kabla ya kuanza kwa mechi dhidi ya timu ya Bunge ya Tanzania .

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeazimia kuondoa wabunge wake katika timu ya Bunge inayoshiriki michezo ya mabunge ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, uamuzi huo umefikiwa baada ya Kamati Kuu ya Chadema kutathmini hali ya kisiasa nchini.

“TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WABUNGE WA CHADEMA WAJITOA KWENYE TIMU YA BUNGE INAYOSHIRIKI MICHEZO YA MABUNGE YA NCHI ZA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI (EAC)

Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) inayoendelea kukutana Jijini Dar es Salaam tangu Jumatano, katika kikao cha dharura, pamoja na masuala mengine, imeendelea kutafakari kwa kina mwenendo wa hali ya kisiasa nchini na kufanya maamuzi kadhaa.

Kipekee katika agenda hiyo, Kamati Kuu baada ya kupokea taarifa na tathmini ya kina ya uchaguzi wa marudio katika kata 43 uliofanyika hivi karibuni, ambao ulitawaliwa na uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu, vitendo vya kinyama dhidi ya ubinadamu na ukandamizwaji mkubwa wa misingi ya demokrasia na utawala bora, kinyume cha sheria za nchi yetu, vyote hivyo vikilenga kuharibu uchaguzi na kupora matokeo tofauti na matakwa ya wapiga kura;

Na baada ya kujiridhisha kuwa vitendo hivyo vimefanyika kwa makusudi, vikilindwa au kunyamaziwa na mamlaka za kiserikali zenye wajibu wa kusimamia taratibu za uchaguzi, vikiwemo vyombo vya dola, lengo ikiwa ni kutaka kuua siasa za ushindani wa vyama vingi na kipekee kuishughulikia CHADEMA, wanachama, wafuasi, mashabiki na viongozi wake;

Kwa kuzingatia pia misimamo ambayo imekuwa ikioneshwa na chama kilichoko madarakani, wakiwemo viongozi wake na hata wabunge katika matukio ya kinyama yanayofanyika wazi kwa nia ya kuwadhuru wanaChadema, mathalani tukio la kushambuliwa kwa nia ya kuuwawa Mwanasheria Mkuu wa Chama na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili nchini (TLS), Kamati Kuu ya Chama imetoa azimio kwa kauli moja kuwa;

1. Wabunge wote wa CHADEMA ambao ni sehemu ya Timu ya Michezo ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoshiriki michezo ya Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) waondoke mara moja kwenye kambi ya timu hiyo.

2. Wajitoe rasmi kushiriki mashindano hayo ambayo mwaka huu Tanzania ndiyo nchi mwenyeji, yakifanyika jijini Dar es Salaam.

3. Kwamba maagizo hayo yanaanza kutekelezwa mara moja kuanzia usiku wa Jumatano, Desemba 6, mwaka huu, baada tu ya kupitishwa kwa azimio hilo, ambapo Kamati Kuu ilimwagiza Katibu wa Wabunge kuwafikishia wabunge husika maagizo hayo mara moja kwa ajili ya utekelezaji.

Maazimio mengine ya kikao cha Kamati Kuu ambacho bado kinaendelea jijini Dar es Salaam, yatatolewa katika hatua ya baadae kwa njia ambayo umma utataarifiwa rasmi.

Imetolewa na;

Tumaini Makene

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano

CHADEMA.”

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni