Makala Maalumu

Akili yatumika kumdhibiti

Tarehe October 29, 2017

Mchezo wa Young Africans dhidi ya Simba Oktoba 28, 2017 katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Ndio….Ndio…..Ndio…..Akili imetumika. Unaweza kujiuliza akili gani imetumika. 1-1…..Shamba la Bibi….Uhuru jijini Dar es Salaam. Kulikuwa na kitu gani kinaendelea katika ardhi hiyo?

Sio jambo jingine isipokuwa mtanange wa kandanda baina ya watani wa jadi wa Kariakoo jijini humo. Young Africans na Simba SC baada ya miaka 10 ya kucheza kwenye Uwanja wa Taifa sasa walirudi katika dimba ambalo waliliacha ukiwa baada ya kujengwa Uwanja Mkubwa wa Taifa, safari wakiambiwa bila kumung’unya maneno kwamba hawatautumia na imewezekana baada ya wengi kusema haitawezekana.

Kwanini imewezekana ni kwasababu akili zilitumika. Oktoba 28, 2017 haitasahaulika kwa watani hao kwa mara nyingine tena wakitoka sare ya 1-1 huku Shizza Ramadhani Kichuya na Obrey Chirwa wakizifumania nyavu na kuileta sare hiyo ambayo imetoa ahueni kwenye mitaa mbalimbali nchini kutokana na utulivu uliopatikana ghafla kutoka kwa mashabiki wa miamba hiyo mikongwe ya kandanda nchini.

Kabla ya mtanange huo jina la Emmanuel Okwi na Ibrahim Ajibu yalikuwa midomoni mwa mashabiki wa pande zote mbili kutokana na umahiri wa nyota hao kufumania nyavu. Okwi kwa mashabiki wa Simba SC na Ajibu kwa mashabiki wa Young Africans.

Hata makocha wa George Lwandamina wa Young Africans na Joseph Omog wa Simba walijua wazi kuwa ni wachezaji wenye uwezo mkubwa hivyo lazima wafanye maandalizi ya kutosha na yenye akili kwa ajili ya kuwadhibiti.

Lwandamina alimtumia Andrew Vincent ‘Dante’ kumdhibiti Okwi. Dante alitembea mguu kwa mguu na Okwi ambaye kama akili hiyo isingetumika basi kungekuwa na madhara makubwa kwa upande wa wanaJangwani hao.

Juuko Murshid wa Simba na Mzamiru Yassini walikabidhiwa Ajibu alipokuwa katika dimba la kati alikutana na Mzamiru huku akipanda juu kidogo alionana na Juuko hali iliyomsababisha akose raha kama ilivyokuwa katika Ngao ya Jamii Agosti mwaka huu walivyomtumia Salim Mbonde, Mzamiru Yassin na Method Mwanjali.

Yote juu ya yote Dante licha ya kukabidhiwa majukumu hayo alijikuta akimwachia upenyo mdogo Okwi ambaye alitoa pasi muhimu ambayo baadaye Kichuya akaitendea haki na kuipa uongozi Simba. Chirwa naye alitumia akili kumalizia mkwaju murua wa kijana wa kutoka Usafwani huko mkoani Mbeya Geoffrey Mwashiuya kuipa bao zikiwa ni dakika takribani tatu baada ya Simba SC kutangulia kutupia kambani.

Wengi walidhani uwanja ungejaa lakini ilitumika akili tu kuongeza kiingilio na watu walioingia hata hawakufanya uwanja ukose nafasi ya kupita. Wengine walidhani kungetokea vurugu lakini wala. Hapo napo kuna la kujifunza kuwa kumbe inawezekana miamba hiyo kucheza hata kwenye viwanja vidogo na mambo yakaenda kama tunavyoona Manchester United ya England ina mashabiki wengi lakini bado itaifuata Burnley kwenye  uwanja wake mdogo ukilinganisha na Old Trafford na maisha yanaendelea.

Vivyo hivyo kumbe kiburi cha miamba hiyo kwenda Chamazi kucheza na wenyeji wa uwanja huo Azam FC kinafutwa na sasa tutashuhudia miamba hiyo kwenye mechi zake ikienda Azam Complex kucheza na mambo yakaenda, kwani inahitajika akili tu.

Hoja nyingine iliyokuwa ikileta utata kuelekea mchezo huo ilikuwa ni usajili wa miamba hiyo, baadhi walikuwa wakifikiria matumizi makubwa ya pesa katika usajili yangewasaidia kushinda mchezo huo kumbe sio hivyo.

Suala la usajili mkubwa au mdogo sio kigezo kikubwa kwamba dimbani utashinda kila mchezo ulioko mbele yako au utashindwa.  Hata hivyo jambo la kuzingatia katika mechi za watani ni kwamba hakuna tajiri wala maskini, kinachotakiwa ni siku ilivyoamka ndivyo matokeo yatakavyokuwa.

Imetayarishwa na Jabir Johnson

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni