Makala Maalumu

Wanamichezo wanawezaje kutumia mitandao ya kijamii kutengeneza brand zao?

Tarehe October 4, 2017

Mbwana Samatta

Maendeleo makubwa katika Sayansi na Teknolojia katika karne ya 21 yanazidi kukua kila uchao, miaka 20 iliyopita ilikuwa vigumu kwa nchi zinazoendelea kuwasiliana kwa kutumia mitandao ya kijamii.

Haikutosha wakati mitandao ya kijamii ilipoingia katika nchi hizo ikiwamo Tanzania kulikuwa na kasumba ya kuitumia.

Mtu aliyekuwa katika mitandao hiyo alionekana kama muhuni anayekiuka maadili ya kijamii na kujiingiza katika tabia zisizofaa. Kwa upande wa makampuni baadhi yao katika nchi hizo yalikuwa yakiona sio sawa kujikita katika mitandao ya kijamii hivyo hayakuwa na muda wa kutumia fursa hiyo kutangaza bidhaa zao.

Hata ikitokea ukayapelekea proposal ambayo ina uhusiano na mitandao ya kijamii kama facebook, twitter na instagram ilikuwa vigumu kukubalika.

Katika nchi zilizoendelea maendeleo ya kiuchumi yaliwafanya kutumia mitandao ya kijamii kuwa fursa ya kujitangaza.

Kwa sasa nchini Tanzania ambayo ni miongoni mwa nchi zilizoendelea ina idadi kubwa ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wakiwamo wanamichezo.

Lakini swali kubwa kwao hadi sasa wanajua kutumia fursa hiyo kujenga uchumi wao. Katika mchezo wa kikapu Michael Jordan alishastaafu kucheza mchezo huo lakini mpaka kesho ataendelea kufaidi matunda ya kuwekeza kupitia mitandao ya kijamii.

Cristiano Ronaldo

Kwa sasa mwanasoka wa Ureno Cristiano Ronaldo anayeitumikia Real Madrid ya Hispania anaongoza kwa kuwa na wafuatiliaji wengi katika mitandao ya kijamii zaidi ya milioni 120.

Hata kabla alipokuwa Manchester United alikuwa na wafuatiliaji wengi. Lebron James anafuata pia Lionel Messi.

Sio hao tu bali wapo Kevin Durant, Kobe Bryant, Maria Sharapova, Rafael Nadal, Tiger Woods na wengineo. Hata hivyo wanaosakata kabumbu ndio wanaoongoza kwa kufuatiliwa na wengi kuliko michezo mingine.

Nchini Tanzania, Mbwana Samatta anayesakata kabumbu nchini Ubelgiji katika klabu ya KRC Genk ana zaidi ya followers takribani 600,000 (Kwa idadi hiyo nchini Tanzania ni kubwa mno kwa mwanamichezo kama Samatta).

Kuwa na fans wanaokufuatilia kuna faida kubwa katika kutumia fans hao kukua kiuchumi.

Ronaldo katika instagram ana zaidi ya followers milioni 90 jambo ambalo hakuna kampuni duniani ambalo litakataa kutoa ufadhili wake kwa namna yoyote ile.

Jambo la msingi kwa wachezaji wa Kitanzania wanapaswa kujitambua, kuchukua hatua ya kuwa na nidhamu katika fani yao. Mchezaji akiwa na tabia mbaya sidhani kama kutakuwa na kampuni linalotaka kujiingiza humo kuchafua image yake kwa wateja wake.

Aidha makampuni hayo hayo yanapaswa kuacha tabia ya kusubiri mpaka wanamichezo wawafuate, maofisini mwao.

Yanapaswa kujipeleka huko baada ya kufanya utafiti hali ambayo itakuwa chachu kwa wanamichezo wasiojitambua.

Urasimu katika makampuni unapaswa kuzikwa ili kuendana na wakati uliopo. Unakuta kampuni linataka kutumia njia za zamani katika ulimwengu wa kisasa eti kwa kigezo polepole ndio mwendo. Kwa ulimwenguni tuliopo na ujao inatupasa kuacha kuwa na maono ya ndani ya boksi ambayo wakati mwingine hayasaidii kuleta ubunifu zaidi sana yatakuwa yakiibua migogoro kila kukicha kutokana na kuwa na watu ambao hawajisikii vizuri kuona wengine wakiendelea.

Kwa uchache ni kwamba lazima wanamichezo wa Kitanzania wakubali kuwa michezo wanayoicheza hawataicheza milele kuna kipindi kisichozidi miaka 10 katika ubora wao kisha umri utakuwa umewatupa mkono.

Hivyo ni vema kuanza kutengeneza mazingira mazuri wakiwa katika ubora wao ili waweze kuishi kwa amani na furaha baada ya kustaafu kwao.

Isiwe kama baadhi ya wachezaji wa zamani ambao walitumika pasipo kuwa na mawazo kuwa siku moja hawatacheza tena na kujikuta wakifa maskini licha ya kuwa maarufu.

Kwa sasa tunajivunia kuwa na Samatta nchini Ubelgiji pia Farid Mussa kule nchini Hispania na Simon Msuva kule Morocco na wengine waliopo nje ya nchi.

Imetayarishwa na Jabir Johnson.

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni