Makala Maalumu

Maswali sita kwa Ibrahimu Ajibu

Tarehe July 30, 2017

Mchezaji wa Simba Ibrahimu Ajibu (wa kwanza kulia) akimkabidhi mtoto Azizi Gisa ‘Ajibu Jr’ (wa kwanza kushoto) vifaa vya michezo na darasa, katika tukio lililofanyika katika Hoteli ya Golden Crown mjini Dodoma Mei 27 mwaka huu baada ya ahadi ya klabu ya Simba SC kuahidi kumsaidia kijana huyo kutokana na uzalendo aliouonyesha Machi 11, 2017 alipovaa jezi ya Ajibu aliyoichora kwa peni kwenye mchezo dhidi ya Polisi Dodoma. Katikati ni mama mzazi wa Ajibu Jr Theresia Mtusi.

Mchezaji wa Simba Ibrahimu Ajibu (wa kwanza kulia) akimkabidhi mtoto Azizi Gisa ‘Ajibu Jr’ (wa kwanza kushoto) vifaa vya michezo na darasa, katika tukio lililofanyika katika Hoteli ya Golden Crown mjini Dodoma Mei 27 mwaka huu baada ya ahadi ya klabu ya Simba SC kuahidi kumsaidia kijana huyo kutokana na uzalendo aliouonyesha Machi 11, 2017 alipovaa jezi ya Ajibu aliyoichora kwa peni kwenye mchezo dhidi ya Polisi Dodoma. Katikati ni mama mzazi wa Ajibu Jr Theresia Mtusi.

Juni 15, 1964 katika kitongoji cha Frederiksberg jijini Copenhagen nchini Denmark alizaliwa mchezaji mahiri wa kandanda ulimwenguni ambaye kwa sasa ni kocha wa klabu ya Al Rayvan ya nchini Qatar ambayo amesaini kuifundisha miaka miwili ambao alisaini Oktoba 3, 2016.

Mchezaji huyo sio mwingine bali ni Michael Laudrup. Kwa wengi wanaofuatalia kandanda watakuwa wanamfahamu kiungo huyo ambaye yupo katika orodha ya viungo bora wa dunia waliowahi kutokea katika historia ya kandanda katika karne ya 20.

Katika maisha yake ya kandanda alichukua mataji akiwa mchezaji wa klabu kubwa ikiwamo Ajax, Barcelona, Real Madrid na Juventus. Kwenye klabu hizo alifahamika zaidi kwa staili yake ya ushambuliaji licha ya kuwa na uwezo mkubwa pia wa kucheza nafasi nyingine katika ukanda huo wa ushambuliaji.

Rekodi kwa nyota huyo zinaonesha alipokuwa akifikisha miaka 18 alikuwa tayari ameshafunga mabao 37 katika mechi 104. Aliitwa timu ya taifa katika Michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1986  na kuanzia Novemba ya 1994 alipewa unahodha wa timu ya taifa ya Denmark ambayo alihudumu katika nafasi hiyo kwa mechi 28 ikiwamo ile aliyoiongoza kutwaa taji la Kombe la Mashirikisho ya Mabara.

Ajibu wakati akikabidhiwa jezi katika klabu ya Yanga.

Ajibu wakati akikabidhiwa jezi katika klabu ya Yanga.

Tukiachana na maisha yake ya awali aliyoanzia nchini Denmark katika klabu ya baba yake iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Vanlose na baadaye Brondy alipata bahati ya kutua nchini Hispania akitokea Italia katika klabu ya Juventus awali alikuwa Ajax kabla hajatua jijini Turin.

Hakuwa na maisha mazuri ya kandanda akiwa na Biaconneri akaona ni sababu tosha ya kuweza kuondoka  baada ya miaka sita ya kuwa na Bibi Kizee cha Turin.

Mwaka 1989 alijiunga na Barcelona huku akijinasibu kuwa mkongwe Johan Cruyff ambaye alikuwa akipambana wakati huo kuirudisha Barca katika mstari ndiye ‘role model’ wake katika kandanda.

Laudrup alipata mafanikio makubwa akiwa mikononi mwa Cruyff kutokana mbinu ambazo aliwahi kusema zilimsaidia kukuza kipaji chake. Wakati anatua Katalunya alikuwa miongoni mwa wachezaji watatu wa kigeni walioruhusiwa kucheza katika kikosi hicho.

Alizungukwa na raia wa Uholanzi Ronald Koeman katika safu ya ulinzi na mshambuliaji raia wa Bulgaria Hristo Stoichkov ambao waliunda kile kinachofahamika ‘Johan Cyruff Dream Team’ huku akipewa na wachezaji chipukizi Pep Guardiola, Bakero na Begiristain.

Licha ya kuchukua makombe akiwa na Barcelona, mwaka 1994 Laudrup alikamilisha usajili wa kustaajabisha na kukanganya miongoni mwa mashabiki pale alipoamua kuachana na Cyruff na kukimbilia jijini Madrid huku akijitetea kuwa hakuwa na agenda ya siri.

Mwaka mmoja kabla ya Kombe la Dunia la mwaka 1994 kwa mujibu wa Laudrup alitabiri kuwa Barcelona isingeweza kuchukua mataji makubwa barani Ulaya kutokana na wachezaji wengi kujikuta wakianguka katika ubora wa viwango vyao.

Maneno hayo yaliwakera sana baadhi ya mashabiki wa Barcelona. Hatimaye Laudrup alijiunga na Real Madrid huku akiwa amezungukwa na maneno ‘chungu mbovu’ kuwa alikuwa ameenda Santiago Bernabeu kwa ajili ya kulipiza kisasi kwani wakati huo Los Blancos ilikuwa ikiwa katika harakati za kurudisha makali yake.

Laudrup alikaririwa akisema alikwenda Real Madrid kwasababu alikuwa na njaa ya kutaka ushindi na kwamba Madrid ilikuwa na wachezaji wanne waliokwenda Kombe la Dunia  hivyo itakuwa rahisi kwake kuwa mikononi mwa kocha mpya, wachezaji wapya na kiu ya ushindi miongoni mwao kurudisha makali.

Ukweli ni kwamba alikwenda Madrid hivyo aliiua uimara wa kikosi cha Barcelona msimu ule kwani alipotua alifanikiwa kutwaa taji la tano mfululizo akiwa na klabu mbili tofauti.

Kinachovutia zaidi Laudrup alicheza na El Clasico ya msimu wa 1993-94 akiwa na Barcelona na kuiadhibu Real Madrid mabao 5-0 kisha msimu uliofuata wa 1994-95 kuiadhibu klabu yake ya zamani ya Barcelona kwa mabao 5-0.

Hakika hata ungekuwa mpenzi na mshabiki wa Barcelona ungekasirika sana. Katika uchezaji wake kuwa haraka, kutumia akili na kipaji katika nafasi ya kiungo na kasi ya mpira vilimpa kujulikana sana.

Kubwa zaidi alikuwa na nidhamu katika uchezaji wake kwani hakuwa kupewa kadi nyekundu. Tukirudi nchini Tanzania kwa mashabiki wanaohasimia Simba na Yanga ‘ulisimama’ baada ya dirisha la usajili kufunguliwa kwa ajili ya msimu wa 2017/18 wakishuhudia mchezaji Ibrahim Ajib alipotangaza kuachana na Simba na kwenda kwa mahasimu Yanga.

Aina ya uchezaji wa Ajibu hauna tofauti na ule Laudrup na hata sasa anatua Yanga akiwa nyota na amekutana na nyota wengine wakali ambao watamzunguka katika kutimiza majukuma yake. Sio vibaya nina swali moja kwa Ajibu.

Maswali sita (6) kwa Ajibu

Ibrahim Ajibu

Ibrahim Ajibu

 Ajibu uliyekimbilia klabu ya Yanga unaikumbuka Mei 27 mwaka huu pale Dodoma muda mchache kabla ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (ASFC) ulipomkabidhi zawadi mtoto wa darasa la tano ambaye Machi 11 mwaka huu mtoto huyo alivalia jezi yako namba 23 uliyokuwa ukiitumia ulipokuwa Simba?

Mtoto huyo ambaye sasa anajulikana mtaani kwao kama Ajibu Jr wakati jina lake halisi ni Aziz Gisa unamwacha katika mazingira gani?

Utaendelea kumpa msaada wa hali na mali kama ulivyoahidi siku ile katika ukumbi wa Hotel ya Golden Crown mjini Dodoma?

Utamhamisha kutoka klabu ya Simba kwenda Yanga kama ulivyohama wewe?

Je, mama yako ambaye aliishukuru Simba kwa kukutunza naye ana mtazamo gani kuhusu mapenzi yake kwa Simba SC?

Utaisaidia Yanga kurudisha kichapo cha mabao 5-0 ilichokipata miaka ya hivi karibuni, kichapo ambacho kinaitesa klabu uliyohamia hadi leo?

Nihitimishe kwa kusema sio vibaya kwako kuhama lakini umewaachia majonzi makubwa wapenzi na mashabiki wa Simba kama ambavyo Laudrup aliwaachia majonzi makubwa wapenzi na mashabiki wa Barcelona miaka 23 iliyopita kama jezi yako ulipokuwa Simba namba 23.

Imetayarishwa na Jabir Johnson

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni