Makala Maalumu

Lijue chimbuko la ‘Siku ya Mtoto wa Afrika’

Tarehe June 16, 2017

 

Mtoto Hector Pieterson aliyeuwawa kwa risasi, akiwa amebebwa na mwanafunzi mwenzake na dada yake pembeni.

Mtoto Hector Pieterson aliyeuwawa kwa risasi, akiwa amebebwa na mwanafunzi mwenzake na dada yake pembeni.

Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo imekuwa ikiadhimishwa kila Mwaka, Juni 16 ilianza kuadhimishwa kuanzia mwaka 1976 na Jumuiya ya Umoja wa Afrika.

Katika mwaka huo, kulitokea mauaji ya watoto zaidi ya 100 katika maandamano ya Soweto yaliyolenga kupinga Elimu Duni katika mashule nchini Afrika ya Kusini.

Tukio hilo la mauaji ndilo lilikuwa chimbuko hasa la “Siku ya Mtoto wa Afrika” ambapo kila mwaka siku hiyo inaadhimishwa kukumbuka tukio hilo na kuhakikisha kuwa Mtoto wa Afrika anapata mazingira bora ya kuishi, kukua, kupata elimu pamoja na kuwa na maadili mema.

Ni siku maalumu ya kutambua na kuheshimu utu, thamani na umuhimu wa mtoto katika dunia huku elimu ikipewa kipaumbele ikilenga kumuinua Mtoto wa Afrika kielimu.

Kitaifa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yanafanyika leo Mkoani Dodoma huku kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa, ‘Maendeleo Endelevu 2030: Imarisha Ulinzi na Fursa Sawa kwa Watoto’.

Kauli mbiu hii ni kumbusho kwa jamii kutambua umuhimu wa mtoto na kutoa ulinzi wa kutosha pamoja na huduma muhimu kama lishe bora, elimu, huduma za afya pasipo kuwabagua kwa minajili ya jinsia zao, kipato cha kiuchumi na kiafya.

Suala la ulinzi kwa Mtoto wa Afrika ndio la kutiliwa msisitizo kwani kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Huduma ya Simu kwa Mtoto, watoto ndio wanaoongoza kwa kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo ubakaji, vipigo na mateso, kukosa chakula na malazi, ndoa za utotoni, mimba za utotoni pamoja na kutelekezwa na mzazi mmoja au wote.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, vitendo vya ukatili dhidi ya watoto hufanywa na watu wa karibu kabisa kwa watoto huku wengine wakiwa ni wazazi wao wa kuwazaa.

Ni jukumu la Serikali kwa kushirikiana na wazazi au walezi wa watoto kuhakikisha kunakuwepo na ulinzi wa kutosha kwa watoto wote huku elimu ikipewa kipaumbele kwani kuwekeza elimu kwa watoto ndio njia pekee ya kuweza kufikia malengo endelevu kwa Bara la Afrika na Dunia nzima.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni