Habari/News

Walazimika kula kinyesi chao, damu na mkojo kunusuru maisha

Tarehe January 6, 2017

1

Watu 50 wakiwa na watoto wadogo wamenusurika kufa, baada ya kupotea ndani ya Pori la Akiba la Selous kwa siku saba bila chakula na maji na kulazimika kula kinyesi cha ng’ombe, damu na mikojo ya binadamu.

Watu hao ambao ni wafugaji, walikuwa wakihama na mifugo yao inayokadiriwa kufikia 1,780 kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, yakiwemo Chumvi na Muhoro waliekea Morogoro, ambako walidai ndiko yalipo makazi yao.

Wafugaji hao walisema walitembea kwa siku tano ndani ya pori hilo, wakitarajia kufika Malinyi, yaliko makazi yao lakini hali ilikuwa tofauti, baada ya mwenyeji wao huyo, kuwalaghai kwa kuwapitisha njia sisizo sahihi.

2

Wanasema waliishiwa chakula na maji ya akiba na mwisho walijikuta wanatokea ndani ya Pori la Akiba la Selous; huku hali zao zikiwa zimedhoofu kutokana na njaa na kiu cha maji. Wakiwa safarini, mwenyeji wao huyo, aliwataka kila mmoja alipe fedha ikiwa ni ujira wake kwa kuwaonyesha njia. Walidai kuwa walimlipa fedha nyingi.

Hali ilizidi kuwa mbaya zaidi, baada ya kutimia siku ya tano wakiwa ndani ya pori hilo, pale walipoishiwa chakula na maji, hivyo kuwalazimu kuanza kuchinja ng’ombe na kunywa damu kwa ajili ya kukata kiu na walikula kinyesi chao ili kupunguza njaa.

Yule mwenyeji wao aliwatelekeza baada ya kuona hali zao zimekuwa mbaya na kutokomea kusikojulikana, akiwaacha wasijue pa kwenda, hivyo kulazimika kutelekeza mifugo yao ili kunusuru kwanza maisha yao.

3

Akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika eneo hilo, kiongozi wa jamii hiyo ya wafugaji alisema baada ya kuona hali inakuwa mbaya zaidi, alitafuta eneo ambalo lina mtandao wa simu na kufanya mawasiliano na watu mbalimbali, ambapo alifanikiwa kuwasiliana na watu wa Kigoma na kuomba msaada wao.

Amesema kuwa watu hao, waliwasiliana na wahifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi na kuwasiliana na wahifadhi wa Pori hilo la Selous, ambao walianza kazi ya kuwasaka na hatimaye kuwakuta katika eneo la Mlima Luhombelo, lililopo katikati ya Pori hilo wakiwa tayari wameshadhoofika kiafya.

Askari hao wa wanyamapori wa Pori hilo, waliwapatia uji na maji na kuwapa huduma ya kwanza wale wengine ambao walikuwa na hali mbaya.

Baada ya taarifa hizo za kupotea kwa wafugaji hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Gaudence Milanzi alifika katika eneo hilo juzi, akiambatana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Martin Leibooki, Meneja wa Pori la Akiba la Selous, Henock Msocha na maofisa wengine wa wizara na pori hilo.

Milanzi alisema Serikali inaangalia namna ya kuwasaidia wafugaji hao, kurejea katika hali zao kiafya pamoja na kuwasaidia kutafuta mifugo yao ili waweze kurejea katika makazi yao na kuendelea na shughuli zao.

4

 

 

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni