Habari/News

Viongozi taasisi ya mikopo elimu ya juu wakamatwa kwa utapeli

Tarehe November 15, 2017

Viongozi wa  Taasisi ya Kusaidia Jamii ( TSSF) ambayo ilitangaza kuwa inatoa mikopo ya elimu ya juu wamekamatwa na polisi baada ya kugundulika kuwa ni matapeli.

Waliokamatwa jana jioni ni Wakurugenzi na Watendaji Wakuu wa TSSF, mara tu baada ya mkutano wa waandishi wa habari na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha kuelezea kuhusiana na uchunguzi uliofanyika dhidi ya taasisi hiyo baada ya Mbunge wa Mafinga Mjini (CCM), Cosato Chumi kuomba mwongozo bungeni.

Chumi alitaka ufafanuzi kuhusu uhalali wa taasisi hiyo baada ya kutangaza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa kulipa Shilingi 30 000 kama ada ya maombi ya kusajiliwa kuomba mkopo.

Akijibu muongozo huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema  Serikali haitambui taasisi hiyo na kuahidi kufanya uchunguzi.

Ole Nasha amesema baada ya uchunguzi huo wamebaini kuwa taasisi hiyo haina uwezo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi 50,000 ambao ilitangaza kutoa.

Amesema katika mahojiano na taasisi hiyo viongozi hao walisema kuwa fedha za kuwakopesha wanafunzi hao watazipata kutoka nje ya nchi baada ya kupeleka kiasi cha fedha.

Hata hivyo, amesema mkataba wa taasisi hiyo na wafadhili hao unaonyesha kuwa wamefikia makubaliano ya kufanya utafiti wa jinsi wanavyoweza kukusanya fedha na si kuwapa fedha kwa ajili ya kutoa mikopo huku ikiwa tayari imekusanya fedha kwa wanafunzi 600 na imepeleka wanafunzi 198 katika vyuo mbalimbali nchini kwa makubaliano ada zao wangelipa Desemba mwaka huu.

Amesema hakuna uthibitisho kama wana fedha kweli za kuwalipia wanafunzi hao ada ingawa wanadai kuwa katika akaunti zao za benki wana fedha kati ya Shilingi milioni 600 na 700.

Mbali na kukamata wakurugenzi na watendaji hao, ameagiza pia akaunti zao zote kufungiwa hadi hapo watakapomaliza uchunguzi sambamba na taasisi hiyo kutojihusisha na shughuli yoyote.

Baada ya kumaliza mkutano huo polisi kutoka makao makuu ya polisi waliingia ndani ya ukumbi wa mkutano na kuwaeleza wako chini ya ulinzi na kuwakamata na kuondoka nao.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni