Habari/News

Sheikh Ponda apewa siku 3 kujisalimisha polisi kwa uchochezi

Tarehe October 12, 2017

Sheikh Ponda.

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imemtaka Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda kujisalimisha ndani ya siku tatu kuanzia leo Alhamisi kwa kosa la kutoa lugha ya uchochezi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Lazaro Mambosasa amesema  ni vyema Sheikh Ponda akajisalimisha kabla hajatafutwa.

Mambosasa amesema jana Jumatano Sheikh Ponda alitumia lugha ya uchochezi alipozungumza na waandishi wa habari na kutoa kejeli kwa Serikali.

Mapema jana, Sheikh Ponda aliitisha Mkutano na Waandishi wa Habari kwa ajili ya kuzungumza mambo kadhaa kuhusiana na hali ya Mbunge wa Singida Mashariki(Chadema), Tundu Lissu na kuelezea namna alivyomtembelea hospitali Jijini Nairobi na kuzungumza naye.

Sheikh Issa Ponda alisema kuwa aliguswa na hisia za Mbunge huyo ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (TLS), pale alipokwenda kumtembelea hospitalini Nairobi alipolazwa akiendelea kupatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa kupigwa risasi.

Ponda alisema hali Lissu inaednelea vizuri na kwamba hivi karibuni atarudi katika harakati zake na kuanzia pale alipoishia.

Alisema madhumuni ya safari yake yalikuwa kumjulia hali Lissu, kumwombea dua, kumjengea matumaini ya afya na kujenga mazingira mapana yanayotosha kulizungumza jambo lililomfika kwani hata yeye mwaka 2013 alipigwa risasi, lakini mwaka huu amepigwa Lissu na kuomba wananchi wajitokeze kukemea matukio kama hayo.

“Tulipokuwa tunabadilisha mawazo, niliguswa na hisia kubwa, badala ya mimi kumpa matumaini yeye ndiye alinipa matumaini,” alisema Ponda.

Aidha, alisema Mhe. Lissu amehimiza mshikamano kuonesha kuwa ana matumaini na Watanzania kwa harakati wanazozifanya.

Awali, Jeshi la Polisi jana lilifika katika eneo la mkutano huo ulioandaliwa Sheikh Ponda na kuwakamata baadhi ya waandishi wa habari huku Sheikh Ponda akifanikiwa kuondoka.

Kamanda Mambosasa amesema kukimbia kwake hakutasaidia chochote hivyo ni vyema ajitokeze kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu suala hilo.

“Sheikh Ponda alikuwa anajua kwamba anafanya kosa kwa sababu aliwaambia waandishi waje saa nne yeye akawapigia baadhi waje kabla ya saa nne,’’ amesema.

Kamanda Mambosasa amesema baada ya askari kufika eneo ambalo Sheikh Ponda alikutana na waandishi wa habari,  waliwachukua waandishi na wafuasi wake kwa mahojiano ambapo baadae waliachiwa huru.

Lissu alijeruhiwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, mwaka huu akiwa nyumbani kwake Area D Mjini Dodoma majira ya mchana akiwa anatoka Bungeni.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni