Habari/News

Sheikh Ponda ajisalimisha Polisi

Tarehe October 13, 2017

Sheikh Ponda.

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa asubuhi hii amefika katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano akiwa na jopo la Wanasheria wakiongozwa na Profesa Abdallah Safari.

Hatua ya Sheikh ni muitikio wa wito uliotolewa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam hapo jana ukimtaka kufika kituoni hapo kwa mahojiano ukimtuhumu kwa uchochezi.

Mapema jana, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ilimtaka Kiongozi huyo kujisalimisha ndani ya siku tatu kuanzia jana Alhamisi kwa kosa la kutoa lugha ya uchochezi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Lazaro Mambosasa alisema kuwa  ni vyema Sheikh Ponda akajisalimisha kabla hajatafutwa.

Mambosasa alisema juzi Jumatano Sheikh Ponda alitumia lugha ya uchochezi alipozungumza na waandishi wa habari na kutoa kejeli kwa Serikali.

Sheikh Ponda aliitisha Mkutano na Waandishi wa Habari kwa ajili ya kuzungumza mambo kadhaa kuhusiana na hali ya Mbunge wa Singida Mashariki(Chadema), Tundu Lissu na kuelezea namna alivyomtembelea hospitali Jijini Nairobi na kuzungumza naye.

Sheikh Issa Ponda alisema kuwa aliguswa na hisia za Mbunge huyo ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (TLS), pale alipokwenda kumtembelea hospitalini Nairobi alipolazwa akiendelea kupatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa kupigwa risasi.

Ponda alisema hali Lissu inaednelea vizuri na kwamba hivi karibuni atarudi katika harakati zake na kuanzia pale alipoishia.

Alisema madhumuni ya safari yake yalikuwa kumjulia hali Lissu, kumwombea dua, kumjengea matumaini ya afya na kujenga mazingira mapana yanayotosha kulizungumza jambo lililomfika kwani hata yeye mwaka 2013 alipigwa risasi, lakini mwaka huu amepigwa Lissu na kuomba wananchi wajitokeze kukemea matukio kama hayo.

“Tulipokuwa tunabadilisha mawazo, niliguswa na hisia kubwa, badala ya mimi kumpa matumaini yeye ndiye alinipa matumaini,” alisema Ponda.

Aidha, alisema Mhe. Lissu amehimiza mshikamano kuonesha kuwa ana matumaini na Watanzania kwa harakati wanazozifanya.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni