Habari/News

Serikali yaja na kauli mpya kuhusu ‘Bunge Live’

Tarehe November 11, 2017

Serikali imesema kuwa mtu yeyote ama taasisi yenye pesa ya kurusha matangazo mubashara ya Bunge ‘live’ ajitokeze ili apewe utaratibu wa kufanya hivyo.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe katika mahojiano na kituo kimoja cha luninga nchini baada ya kuulizwa kuwa Serikali ilidai gharama za kurusha bunge live ni kubwa sana wakati taasisi mbalimbali ikiwemo Tanzania Media Fund (TMF) zilidai kuwa zipo tayari kulipia gharama za kuonesha matangazo mubashara ya bunge.

Dkt. Mwakyembe amesema Serikali ya Awamu ya Tano imekuja na sera ya kuhakikisha kuwa kila fedha inayopatikana inatumika pale inapohitajika na kudai kuwa hatahivyo kipindi cha maswali na majibu bungeni kinarushwa mubashara na pale panapokuwa na suala muhimu.

“Niwahakikishie kuwa vipindi vyote vya Bunge ukienda TBC usiku utaviona vyote na mjadala mzima utauona lakini ukisema uweke ‘live’ asubuhi na mchana watu hawatafanya kazi bali kuangalia bunge huku wabunge wanaopenda vijembe wataacha kujadili mambo ya msingi na kutumia mwanya huo kurusha vijembe,” amesema Dkt. Mwakyembe.

Amesema hata taasisi hizo zilizojitokeza awali na kudai kuwa zingelipia matangazo hayo zingekimbia baada ya muda mfupi kutokana na gharama kuwa kubwa sana kwani hata TBC wenyewe hawawezi.

Katika Serikali za Awamu ya Tatu na Nne, Bunge lilikuwa likioneshwa mubashara ‘live’ lakini Serikali ya Awamu ya Tano ilikuja na sera ya kutoonesha matangazo hayo moja kwa moja na badala yake ni kipindi cha maswali na majibu pekee ndicho kinachooneshwa moja kwa moja.

Maamuzi hayo yaliibua minong’ono mingi kutoka kwa wanasiasa hasa kutoka upinzani, taasisi na mashirika kadhaa ya wanaharakati wakidai kuwa ni haki ya Watanzania kuona moja kwa moja kile wawakilishi wao wanachofanya na kuzungumza ndani ya bunge.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni