Habari/News

Serikali kufanya mnada wa madini ya Tanzanite

Tarehe October 13, 2017

Serikali kupitia Wizara ya Madini inatarajia kufanya mnada wa madini ya Tanzanite kutoka kampuni nne za uchimbaji na biashara ya madini eneo la Mererani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.

kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Kaimu Kamishna Msaidizi (Uchumi na Biashara ya Madini), Godleader Shoo, mnada huo utafanyika Oktoba 15 na utashirikisha wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi.

Shoo amesema utaratibu wa kufanya mnada huo ni jitihada za Serikali za kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo nje ya nchi na pia kuwasaidia wachimbaji kuuza madini yao kwa bei ya ushindani inayoendana na soko la dunia.

Amesema atakayenunua madini hayo katika mnada ni yule atakayeshinda bei iliyowekwa.

Amezitaja kampuni zitakazouza madini katika mnada huo kuwa ni TanzaniteOne, Franone, Glitter Germs na Classic Gems.

Shoo amesema mnada utafanyika kwa uwazi kwa kushirikisha wachimbaji, wanunuzi, Shirika la Madini la Taifa (Stamico), vikosi vya ulinzi na usalama, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro na Wizara ya Madini.

Hivi karibuni akiwa katika eneo hilo la Simanjiro, Rais, Dkt. John Pombe Magufuli aliagiza madini ya Tanzanite yauzwe katika eneo hilo pekee na sio sehemu nyingine yoyote ile duniani.

Adha, aliagiza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuchukua jukumu la kujenga ukuta mkubwa kuzunguka eneo hilo la madini kuanzia Block A hadi D na kuchukua jukumu la kulinda madini hayo dhidi ya wachache wanaotumia ujanja ujanja kuiba na kutorosha madini hayo na kuikosesha Serikali mapato makubwa.

Madini ya Tanzanite ni madini yanayopatikana Tanzania pekee ulimwenguni lakini kwa muda mrefu sasa wauzaji mashuhuri wa madini hayo wamekuwa ni India na Kenya, ilhali mataifa hayo hayana madini ya Tanzanite.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni