Habari/News

Polisi, TCRA zafunguka kuhusiana na Mange Kimambi

Tarehe December 3, 2017

Mange Kimambi

Jeshi la Polisi limetaka liachwe liendelee kufanya kazi yake kwa weledi katika kushughulikia suala la Mtanzania aishiye nchini Marekani, Mange Kimambi, ambaye anatuhumiwa kuchapisha taarifa zinazodaiwa kuwatusi watu mbalimbali wakiwamo viongozi katika mitandao.

Kwa siku mbili sasa akaunti ya Mange Kimambi ya Instagram haipo hewani.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa, amenukuliwa akisema kuwa ni kweli jeshi lao linalifanyia kazi suala hilo.

“Hili jambo lina mambo mengi sana. Watu wengi wanahusika na taasisi nyingi (pia) zitahusika kulishughulikia, Hivyo tunaendelea kupokea mawazo ya watu mbalimbali kuhusu namna ya kwenda nalo. Mawazo wanayotupa tunayafanyia kazi lakini naomba mtuache kwanza tunaendelea kulishughulikia,” amesema Mwakalukwa.

Wakati huohuo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema kuwa haiwezi kufunga wala kuingilia akaunti ya  Mange Kimambi kwa sababu huo siyo wajibu wake kisheria.

Msemaji wa TCRA, Semu Mwakyanjala, amenukuliwa akisema kuwa mamlaka yao haina nguvu za kisheria kufanya kazi hiyo bali wenye wajibu wa kufanya hivyo ni kitengo cha kudhibiti uhalifu wa mitandaoni cha Jeshi la Polisi.

Amesema  makosa yote yanayohusu mitandao, yakiwamo ya watu kutishiwa maisha, kutukanwa, kuibiwa kwa njia ya mtandao au kunyanyaswa kwa namna yoyote mtandaoni, wanaohusika ni polisi na siyo TCRA.

“Masuala ya akaunti za watu kwenye mitandao kama hiyo unayosema (ya Kimambi)… mwenye mamlaka ya kuingia na kuzifunga ni Jeshi la Polisi. Bunge liliipa mamlaka ya kisheria polisi kuchunguza na kukamata wahalifu kama hao… waulizeni wao,” amesema Mwakyanjala.

Hata hivyo Mange amedaiwa kuibuka kwa akaunti nyingine na kudai kuwa kilichotokea ni matokeo ya kazi ya wadukuzi wa mitandaoni, maarufu kama ‘hackers’ kupoteza akaunti yake yenye wafuasi takribani milioni 1.5.

Pamoja na hayo upo ujumbe wa lugha ya kigeni uliokuwa ukisambaa kwenye mtandao wa instagram ukionyesha kuwa akaunti inayofahamika kuwa ni ya Kimambi, imefungwa na waendeshaji wa mtandao wa Instagram kwa sababu ya kuwapo kwa malalamiko dhidi ya machapisho ya akaunti hiyo.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni