Habari/News

Neno la Mama Anna Mghwira kuhusu njaa nchini

Tarehe January 12, 2017

Mgombea wa ACT – Wazalendo, Anna Mghwira.

Mgombea wa ACT – Wazalendo, Anna Mghwira.

Kwa nini Tanzania ina Njaa?

Anna Mghwira

Njaa inainyemelea Tanzania. Maeneo mengi ya nchi yetu, yana kila dalili ya kuwa na upungufu wa chakula. Ukame uliojitokeza musimu huu unaongeza hofu hii ya kukabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula. Changamoto moja kuu ya suala la chakula ni athari zake kwa raia na watawala moja kwa moja. Ni jambo linalounganisha ama kubomoa jamii.

Makala haya yamezungumza na baadhi ya wazee wa kimila wa maeneo tofauati nchini na kupata majibu tofauti kutoka kwao kuhusiana na hali hii ya uwezekano wa kukutana na njaa kali itakayotikisa taifa.

Mzee mmoja kutoka Sepuka Singida ametoa maoni yake kuwa kimila si kila ukame uliashiria njaa. Wakati mwingine ilikuwa ishara ya shibe mbeleni. Njaa halisi kwa maelezo ya mzee huyu ilitokana na mafuriko yaliyozoa chakula, mimea na akiba za chakula zilizokuwepo. Lakini pia wakati mwingine mafuriko yalikuja baada ya ukame mkali, kwa hiyo kusababisha njaa. Hatujui ukame wa mwaka huu utatuacha wapi. Watabiri wa hali ya hewa wanaweza kutusaidia kujiandaa.

Kuna utamaduni miongoni mwa jamii zetu unaoonesha thamani ya chakula. Mtu akionekana kuwa na maringo yasiyo na sababu sana (hata yenye sababu kama utajiri, ujuzi Fulani wa tofauti nk) watu humnanga anayeringa kuwa kama haleti mvua ama shibe anaringa nini? Ikitokea mwanamke ana maringo sana aliambiwa unaringa hivi unakamuliwa? Unaleta maziwa wewe? Kama huleti mvua ama hukamuliwi unaringia nini?

Semi hizi ziliashiria umuhimu wa chakula, shibe na kujitosheleza: kuwa kama yuko mtu anaweza kuwashibisha wengine, basi huyo anaweza kuringa, kujisikia bora kuliko wengine. Semi hizi pia ziliashiria ubaya wa kukosa chakula, kukosa kujitosheleza na ubaya wa kudhalilika kwa madhila ya kutojitosheleza kwa namna yoyote ile.

Suala la chakula ni suala mtambuka. Lina sura nyingi na linabeba taswira kubwa zaidi ya kukosekana ama kupatikana kwa chakula tu. Jambo hili linahusisha jamii na mtu mmoja mmoja, viongozi wa ngazi mbalimbali, tawala, sera, sheria na taratibu zingine.

Watafiti wana kanuni moja wanayotumia katika kutafuta majibu ya maswali yao. Kanuni hii inataka mtafiti kuuliza maswali sahihi akitaka kupata majibu sahihi kwa maswali yake. Swali sahihi kwa kila suala lina uwezekano wa kutoa jibu sahihi.

Kwa hiyo tunaposhughulikia suala hili ni lazima kujiuliza maswali kadhaa: Je kuna upungufu wa chakula? Je upungufu huu unasababishwa na nini? Je, tuna suluhu ya njaa ya sasa? Na je ni nini suluhu ya kudumu ya tatizo hili?

Mwaka 2015 kikao cha mashauriano katika mkoa mmoja kilikaa na kujadili pamoja na mambo mengine suala la njaa. Swali kubwa juu ya suluhu ya tatizo lilikuwa: tupate wapi chakula. Kikao kilielekezwa kuangalia maeneo mbalimbali kunakoweza kupatikana chakula: Ruvuma, Iringa, Rukwa ama kutoka ghala la taifa.

Swali la msingi hata hivyo wakati wa upungufu wa chakula ni kwa nini kuna njaa, na kama chakula kikipatikana watu wenye njaa watamudu kukinunua? Ama watapewa bure? Swali si kunapatikana wapi chakula, bali uwezo wa watu kukimudu chakula kilichopo na kitakacholetwa.

Swali la kwanza ni gumu, na watu hawapendi kujiuliza maswali magumu. Majibu rahisi kwa maswali magumu pia ni fedheha. Kwa hiyo, kwa nini njaa ipo? Kwa nini watu wenyewe hawakitafuti hicho chakula na kwa nini wasaidiwe kukipata?

Jibu rahisi ni kuwa watu hupata njaa kwa sababu ya kukosekana uwezo wa kujipatia chakula. Hii ndio sababu ya kwanza ya kuwa na njaa, na mtu akitaka kuondoa njaa atengeneze mazingira ya watu kujipatia chakula wakati wote.

Njaa haipo kwa sababu ya aina ya mazao ama kiwango cha mvua kinachopatikana, ama ukame ama mafuriko. Hivyo ni vionjo vya njaa, si viini vyake. Tutatue tatizo la njaa kwa kushughulikia viini vyake kwa kuondoa vikwazo vya watu kujipatia chakula chao wakati wote.

Kwa kuwa sasa tuko kwenye njaa inalazimu kuweka malengo ya muda wa sasa, wa kati na wa kudumu. Kwa sasa tunaweza kutafuta chakula cha msaada kwa waathrika wa njaa, kisha tuweke malengo ya kuondokana na njaa kwa mwaka ujao na miaka mingine ijayo.

Njaa nyingi duniani hutokea kwa sababu ya udhaifu wa muunganiko wa kiutendaji kati ya sekta mbalimbali na katika matumizi ya sera, sheria na kanuni. Kwa hiyo kwa hapa kwetu, ukinzani wa taarifa za njaa kati ya msimamo wa serikali na msimamo wa taasisi yake ni sehemu ya kiini cha tatizo.

Bodi ya takwimu ilipotoa angalizo kuwa uzalishaji wa mahindi kwa mfano ulishuka mwaka 2015 kwa asilimia 8% ikilinganishwa na mwaka 2014, ilitaka kutuamsha kuwa tuna uwezekano wa kukosekana chakula mwaka 2016 / 17. Hotuba ya waziri wa Kilimo bungeni mwaka jana kuwa hali ya chakula ni shwari ilitakiwa kusomwa katika macho ya taarifa ya Bodi, si kinyume chake. Ili kutoa tahadhari. Tahadhari ya sasa tukiwa ndani ya hali yenyewe si rahisi kutekelezeka: Kutunza chakula wakati hakipo!

Viini vya msingi katika sekta ya kilimo na chakula ni kama vifuatavyo: kwanza ni upungufu / uhaba wa pembejeo, kupatikana kwa pembejeo baada ya msimu wa kilimo kupita. Pembejeo za uvuvi na ufugaji nazo pia huja kwa kuchelewa. Hili ni tatizo la muda mrefu la sekta hii ya kilimo, uvuvi na ufugaji. Suluhu yake ni kuwaachia wazalishaji wa kila sekta waunde ushirika wao, waweke mipango yao na kujihakikishia upatikanaji wa pembejeo wanazohitaji kwa wakati.

Kwa njia ya ushirika tunaweza kutatua si tu tatizo la pembejeo lakini pia kupunguza migogoro miongoni mwa wazalishaji wa bidhaa za kilimo na za ufugaji kwa mfano.

Tatizo lingine ni uhaba wa masoko kwa bidhaa za kilimo, ufugaji na uvuvi. Hii inatokana na kwa sehemu utamaduni wa nyuma ambamo serikali ilifanya biashara zaidi kuliko watu binafsi. Hili limelemaza wafanya biashara kukosa nguvu na ujasiri wa kujitafutia masoko na kujiridhisha nayo kibiashara.

Tokeo la masoko ndilo linaloletea kuoza kwa chakula maeneo kadhaa ya nchi wakati maeneo mengine yakikosa chakula. Kwa hiyo kuthibitisha nadharia moja kuwa kwa kawaida njaa hutokea mahali penye chakula upande mmoja wa nchi kwa kukosekana muunganiko wa hiari wa sekta zinazohusika na masuala ya chakula, utawala, mawasiliano na utashi wa kisiasa.

Kwa hiyo kwa mfano njaa kubwa zilizowahi kutokea duniani katika nchi za Ethiopia na Ireland kwa mfano, zilitokana na kukosekana muunganiko wa kiuongozi katika sekta za chakula, na kukosekana taarifa sahihi juu ya hali ya njaa. Hii ndio athari ya moja kwa moja kwa utawala kunapotokea upungufu wa chakula.

Majuzi tumeshuhudia hapa kwetu mwandishi wa habari akiadhibiwa kwa kutoa taarifa ya upungufu wa maji ya umwagiliaji wilayani Arumeru. Aina hii ya maamuzi inachangia kuongeza upungufu wa chakula. Wanasiasa wanatakiwa kujua jinsi ya kutumia taarifa za kitaalam kutatua matatizo ya kitaalamu na kisiasa, si kuzizuia taarifa hizo wala kuwawajibisha watoa taarifa.

Kukosa taarifa sahihi kwa viongozi kunaathiri maeneo mengi ya maamuzi. Tunaweza kuondoa mgongano wa kimasilahi kati ya makundi haya mawili kwa kupanua wigo wa mawasiliano katika sekta za uzalishaji na usambazaji (masoko) chakula.

Ziko changamoto zingine zinazoletea hali ya njaa kushamiri. Hizi ni pamoja na kupungua ama kukosekana kwa usindikaji na ukaushaji wa chakula, wakulima kukopwa mazao, upungufu wa mabwawa, malambo na majosho ya mifugo, uwekezaji mdogo katika sekta za uzalishaji chakula na uwekezaji mdogo wa ki-elimu ya chakula, na lishe.

Kubadilika kwa mitaaala na kuondoa baadhi ya masomo ya msingi katika tasnia ya chakula, biashara na masoko ya bidhaa hizi nk.

Tutaendelea kujadili eneo la pilli la mjadala huu.

Anna Mghwira ni Mwenyekiti wa ACT – WAZALENDO. Ni muandishi na mtafiti wa masuala ya maendeleo kwa kutumia sheria ya haki za binadamu. Anapatikana kupitia barua pepe: aemghw@gmail.com.

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni