Habari/News

Mwigulu ampa za uso Lissu sakata mchanga makinikia

Tarehe June 19, 2017

Mwigulu-Nchemba

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ‘amemvaa’ Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kwamba amejaribu kutengeneza kila aina ya kichaka kukwamisha jitihada za Rais John Magufuli kupambana na usafirishaji holela wa madini nje ya nchi bila mafanikio.

Mwigulu amesema hayo alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Zinzirigi kilichopo katika Jimbo lake la Iramba Magharibi ambapo licha ya kumtaja jina mbunge huyo wa Singida Mashariki, hoja nyingi alizogusia ni zile ambazo Lissu amekuwa akinukuliwa akizisema.

Moja ya hoja hizo ni ile ambayo Mwigulu alisema watu wenye nia mbaya walianza kusema kuwa Serikali itashtakiwa kwa hatua yake ya kuzuia makontena 277 ya mchanga wenye dhahabu.

“Baadaye watu haohao walisema tena kwamba mchanga ule ni takataka tu lakini walipoambiwa wasisafirishe mchanga huo wenye madini walisema wanapata hasara ya Shilingi  trilioni 4 kwa siku,” aliongeza.

Pia, Mwigulu alisema tangu Rais Magufuli alipounda kamati mbili kufuatilia suala la mchanga huo wa madini, watu hao aliowaita kuwa ni wenye nia mbaya walianza kutumia majina ya marais wastaafu Jakaya Kikwete na Benjamin Mkapa kama kichaka ili Serikali iache kufuatilia sakata hilo la mchanga wa madini.

“Hawa watu walikuwa wanatuona kama mazuzu hivi. Rais wetu amechukua hatua tena siyo kwa maneno, kwa vitendo. Tumuunge mkono,” alisema Mwigulu.

Tangu kuanza kwa sakata hilo la mchanga wa madini, Lissu amekaririwa mara kwa mara akisema kwamba suala hilo linashughulikiwa kisiasa badala ya kisheria jambo linaloiweka Tanzania katika hatari ya kushtakiwa na kushindwa.

Pia alikaririwa bungeni akisema Rais Kikwete anaponaje katika sakata hilo na alipoulizwa kuhusu kauli hiyo ya Nchemba alisema msimamo wake uko palepale kuhusu sakata hilo.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni