Habari/News

Mbowe amnyooshea kidole Prof. Lipumba

Tarehe November 14, 2017

Prof. Lipumba (kushoto) akiwa na Freeman Mbowe (kulia) wakati wa bunge la katiba wakijulikana kama viongozi wa Ukawa..

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mhe. Freeman Mbowe amesema Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Prof. Ibrahim Lipumba kuwa ni Profesa wa ajabu ambaye anaweza kubomoa chama alichokijenga.

Mhe. Mbowe amesema hayo akiwa katika kampeni za uchaguzi mdogo Mkoani Mtwara na kudai kuwa hana ugomvi wowote na Prof. Lipumba ingawa amekiri atakuwa muongo akisema kwamba anamuheshimu kwani anatumika katika kukivuruga chama alichokuwa akikiongoza kwa muda mrefu.

Amesema kwamba wakati CUF ikishirikiana na UKAWA kwa ujumla kutafuta kura na kuongeza wabunge wa chama hicho bungeni, Prof. Lipumba alikuwa mafichoni na anamshangaa sasa hivi anavyorudi ndani ya chama hicho na kutaka kukisambaratisha.

“Sina ugomvi na Prof. Lipumba lakini nikisema namuheshimu nitakuwa muongo sana. Prof Lipumba ni msomi sana tena msimchezee kwenye elimu lakini usomi ni jinsi unavyotumia elimu yako lakini siyo wingi wa vyeti. Ni Profesa wa ajabu kweli kweli. Mimi simuogopi mtu nitazungumza ‘straight’,” amesema Mbowe.

Aidha, Mbowe amedai kwamba Spika wa Bunge pamoja na Msajili wa vyama vya siasa wanatumika vibaya katika kuibomoa CUF na kuongeza kwamba hataacha kusema ukweli kwani hakuna mtu yoyote anayemuogopa isipokuwa Mungu pekee.

Ameongeza kwamba kasi inayotumika kuibomoa CUF inatumika pia kuibomoa CHADEMA na kuweka wazi kuwa hilo litatokea siku ambayo atakuwa mfu lakini si wakati huu akiwa hai.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni