Habari/News

Ma ‘Admin’ makundi ya WhatsApp waonywa

Tarehe October 13, 2017

Jeshi la Polisi Kitengo cha Makosa ya Mtandaoni, limewataka viongozi wa makundi ya WhatsApp kuwa makini na makundi yao ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa pindi uhalifu unapofanyika kwenye makundi yao.

Naibu Mkuu wa Kitengo cha Makosa cha ya Mtandaoni, Joshua Mwangasa amesema hayo leo  wakati wa semina iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) na kuwakutanisha viongozi wa dini wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema kufanya hivyo kutasaidia polisi kuchukua hatua dhidi ya mhusika aliyefanya uhalifu ili kukabiliana na ongezeko la vitendo vya uhalifu wa mtandaoni na kwamba makosa ya kimtandao yameendelea kuongezeka kwa kasi kubwa huku makundi ya WhatsApp yakionekana kuwa kichocheo kikubwa.

Mwangasa amesema viongozi wa makundi hayo hawatakiwi kuvumilia makosa hayo hivyo wanatakiwa watoe taarifa polisi.

“Usikubali umeanzisha kundi kwa nia nyingine halafu mtu au watu wanaweka mambo yasiyofaa, toa taarifa hatua zichukuliwe kinyume na hapo hata wewe utahusika,” amesema.

Ameongeza kuwa kwa kiasi kikubwa makundi hayo yamekuwa yakitumika kusambaza taarifa za uongo na uchochezi.

Aidha, Mwangasa ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini kuwahubiria waumini wao juu ya matumizi sahihi ya mitandao ili kujiweka mbali na uhalifu.

“Ukosefu wa maadili ndio unachangia yote haya, ndiyo sababu narudi kwenu viongozi wa dini wasisitizeni waumini wenu watumie mitandao kwa maendeleo,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TCRA, Mhandisi James Kilaba, amesema mamlaka hiyo inaendelea kuchukua hatua kuimarisha ulinzi wa mawasiliano mtandaoni.

Amesema simu za mkononi kwa sasa zimekuwa kama silaha hivyo matumizi yake yanapaswa kuangaliwa kwa umakini zaidi.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni