Habari/News

Kanisa Katoliki lagoma kumzika bilionea Mrema, sababu hii hapa

Tarehe August 10, 2017

Moja ya Kanisa Katoliki nchini.

Moja ya Kanisa Katoliki nchini.

Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha jana lilikataa kuendesha misa ya mazishi kwa ajili ya marehemu, Faustine Mrema, mmiliki wa hotel za Ngurdoto, Impala na Naura springs kwa madai kuwa hakuwa na sakramenti ya ndoa na mke wake wala kipaimara.

Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mt. Theresia, Mtoto Yesu, Jimbo Kuu la Arusha, Padri Festus Mangwingi amethibitisha hilo na kusema marehemu hakuweka heshima kwa kanisa.

“Marehemu ni mkatoliki wa kuzaliwa lakini hakuwahi kuwa na sakramenti ya ndoa na mke wake aliyezaa nae watoto, wala kupata kipaimara hivyo kanisa haliwezi kabisa kumzika. Kwa kawaida, mazishi ya Kanisa Katoliki hutolewa tu kwa mkristu anayestahili. Huyu marehemu hakuwahi kufunga ndoa kanisani na alijitenga na kanisa,” amesema.

Ameongeza kuwa kusema kuwa Kanisa limemtenga si kweli kwani yeye ndiye alilitenga kanisa, hakutaka kuonesha heshima yake kwa kanisa kama mkristu na kuongeza kuwa marehemu hakuwahi kuhudhuria misa za jumuiya ambazo ni muhimu kwa Mkristu.

“Jumuiya ni utaratibu wa Kanisa unaowataka waumini wawe na usharika wa karibu na kufahamiana. Marehemu alikuwa hashiriki kabisa kwenye jumuiya sasa unaanzaje kumzika mtu kama huyo kwa heshima za Kanisa Katoliki?,” alihoji padri Mangwingi.

Baada ya Kanisa hilo kujivua, ilibidi Askofu Dr. Eliud Issangya wa Kanisa la Kimataifa la Kiinjili kuokoa jahazi na akaendesha ibada hiyo ya mazishi iliyofanyika hoteli ya Ngurdoto, wilaya ya Arumeru, Arusha na kuhudhuria na watu wengi wakiwemo viongozi kama Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu wa Zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, Edward Lowassa pamoja na Katibu Mkuu CCM, Abdulrahman Kinana.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni