Habari/News

Kafulila kufunga ndoa na Chadema tena jimboni kwake

Tarehe January 5, 2017

Mhe Kafulila akihutubia maelfu ya wakazi wa Nguruka mara baada ya kuchukua fomu.

Aliyekuwa  Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, amesema atapokea kadi ya Chadema jimboni mwake baadaye mwezi huu baada ya kukihama chama chake cha NCCR-Mageuzi na kutimkia Chadema hivi karibuni.

Kafulila aliamua kurudi Chadema kwa kile alichoeleza kuwa ndicho chama kilichojipambanua kuelekea safari ya mabadiliko ifikapo mwaka 2020.

Kada huyo tayari amewasilisha barua kwa Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe kumjulisha kuwa anajivua uanachama na  anarudi Chadema.

Kafulila amesema ameamua kuwa atapokelea kadi hiyo jimboni kutokana na mapenzi aliyonayo kwa wananchi wake.

“Nimepanga kuchukua kadi mwezi huu jimboni, kwa kuwa ilikuwa nichukue kadi mwanzoni lakini ilishindikana kutokana na siku kuu, hivyo siku yoyote kuanzia sasa nitachukua,” amesema.

Wakati anajiuzulu NCCR-Mageuzi na kurudi Chadema, alisema hakufanya uamuzi kwa kukurupuka bali alitafakari na kushauriwa na wananchi wa jimbo lake, na kuridhika kurudi huko.

Novemba 10, 2009 Kafulila alijivua uanachama wa Chadema na kuhamia NCCR-Mageuzi kutokana na kuondolewa kwenye nafasi ya uafisa habari wa chama hicho.

Pia akiwa NCCR-Mageuzi, alitimuliwa uanachama kwa kudaiwa kukiuka taratibu za chama hicho na tuhuma za kutaka ‘kumpindua’ Mwenyekiti, James Mbatia.

Hata hivyo, suala hilo lilipata suluhu baada ya Mbatia kuteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuwa Mbunge ambapo wakiwa bungeni wawili hao walikutana, kuzungumza na hatimaye kumaliza mzozo wao.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni