Habari/News

Jeshi la Zimbabwe ladhibiti kituo cha taifa cha luninga, ZBC

Tarehe November 15, 2017

Jeshi la Zimbabwe likitumia kituo cha luninga cha Taifa, ZBC kutangaza kuwalenga wahalifu.

Jeshi la Zimbabwe limesoma taarifa katika kituo cha luninga cha Serikali cha ZBC, likisema kuwa linachukua hatua ya kuwalenga wahalifu na kuwa hayo sio mapinduzi ya kijeshi na Rais Mugabe yuko salama.

Taarifa hiyo ya jeshi imekuja saa kadhaa baada ya jeshi hilo kudhibiti kituo cha ZBC huku milio mikubwa ya risasi ikidaiwa kusikika katika maeneo ya Kaskazini mwa Mji Mkuu Harare mapema leo asubuhi.

Mwanamume mmoja ambaye alikuwa amevaa sare za jeshi alisema kuwa jeshi linataka kukabiliana na watu ambao wanatenda uhalifu unaoleta madhara ya kijamii na kiuchumi nchini Zimbabwe.

“Wakati tutakapomalzia wajibu wetu, tunatarajia kuwa hali itarudi kuwa sawa,” amesema.

Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa Rais Mugabe (93), na familia yake wako salama, ambapo taarifa za awali jana zilidai kuwa amewekwa kizuizini katika Ikulu Jijini Harare.

Hata hivyo taarifa zinasema kuwa wafanyakazi wa shirika hilo la utangazaji ZBC, waliambiwa na wanajeshi hao kwamba hawapaswi kuwa na wasiwasi na kwamba uwepo wa vikosi hivyo ni kwa lengo la kulinda eneo hilo.

Magari ya wanajeshi waliojihami kwa silaha yameonekana yakizagaa katika maeneo mbalimbali Mjini Harare na kuibua wasi wasi wa lolote kuweza kutokea.

Hadi sasa hakuna kauli yoyote iliyotolewa na Rais Robert Mugabe kutokana na hali ya sasa nchini mwake hulu Chama cha ZANU-PF kikimtuhumu Mkuu wa Majeshi, Constantino Chiwenga, kwa hatua yake ya kutangaza kuwa jeshi lipo tayari kuingilia mzozo wa kisiasa unaoendelea katika chama hicho kwa lengo la kulinda wapigania uhuru wa taifa hilo.

Marekani imesema kuwa inafuatilia kwa karibu hali ya Zimbabwe na kutoa rai pande zote kutatua mzozo huo kwa njia ya amani.

Naye Balozi wa Marekani nchini Zimbabwe kupitia ukurasa wake wa Tiwtter amesema kuwa leo watasitisha shughuli za kiofisi ubalozini hapo kutokana na hali halisi ya sasa Mjini Harare.

Balozi wa Zimbabwe nchini Afrika Kusini Isack Moyo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa serikali ipo imara katika jambo hilo na kuzuia uwezekano wowote wa kufanyika kwa mapinduzi.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni