Habari/News

Azikwa na mamilioni ya pesa kwa ajili ya kumhonga Mungu

Tarehe January 10, 2017

home001pix

Hakika hakuna nafsi itakayokwepa kuonja mauti na kila mtu ana fikra zake juu ya siku atakayokutana na Muumba wake katika ile siku ya mwisho ya hukumu juu kulingana na matendo yake hapa duniani.

Lakini katika hali ya kushangaza mtumishi mmoja mstaafu wa Serikali huko Uganda aliamua kuwekeza zaidi ya Shilingi milioni 200 kusudi aweza kuja kuzitumia kumhonga Mwenyezi Mungu siku ya hukumu ili aweze kumsamehe dhambi zake.

Charles Obong, 52 aliyekuwa mfanyakazi katika Wizara ya Utumishi wa Umma tangu mwaka 2006 hadi 2016 anadaiwa kutaka kutumia kiasi hicho cha pesa kuokoa nafsi yake mbele ya Mwenyezi Mungu.

Baada ya kuugua kwa muda mrefu hatimaye siku iliwadia ambapo Desemba 17, mwaka jana Charles aliaga dunia na kuzikwa huko nyumbani kwa mababu zake katika jeneza la kumeremeta linalokisiwa kugharimu shilingi milioni 20.

Inadaiwa kuwa wakati wa uhai wake, moja ya masharti aliyoyaacha katika urithi wake ni kwa mke wake, Ms. Margaret Obong kuhakikisha kuwa anaweka kiasi kikubwa cha pesa katika jeneza lake akipanga kutoa fedha hizo kwa Mwenyezi Mungu kama matoleo ili aweze kusamehewa dhambi zake na kuepuka moto wa milele.

Anadaiwa pia kumuelekeza kaka yake Justin Ngole na dada yake, Hellen Albert  kuwa sehemu ya mashahidi kuhakikisha kuwa mke wake huyo anatekeleza agizo lake na kuhakikisha fedha hizo zinawekwa katika jeneza lake.

Hatahivyo, ndugu, jamaaa na viongozi wa mtaa waliohudhuria mazishi yake wanadai kuwa urithi huo haukuweka wazi dhambi ambazo Obong alitaka kusamehewa.

Mashahidi ambao ni kaka na dada wa Obong wamekiri kushuhudia kaka yao akizikwa na kiasi kikubwa sana cha pesa na mjane wa marehemu akawaeleza wazee wa ukoo wa marehemu kuwa alikodi kampuni maalum ya mazishi kufukua kaburi la mme wake na kuongeza kiasi kingine cha pesa akidai kuwa alikuwa na kiasi kingine cha shilingi milioni 180 alichokuwa akitaka kukiweka katika jeneza la marehemu mme wake.

Hatahivyo katika kikao cha ukoo kilichofanyika siku ya Jumamosi Chifu Okii wa Koo ya Okabo iliamriwa mwili huo wa marehemu ufunuliwe na pale wana ukoo walipoanza kuufunua, Ms Obonga akakataa kuwasilisha kiasi cha milioni 180 alizokuwa anataka kuziongezea na badala yake anadaiwa kuingia katika gari yake na kuondoka kuelekea mji mwingine.

Mwenyekiti wa Kaunti ndogo ya Aromo, Bwana David Elic ambaye pia ni shemeji wa marehemu amekiri kushuhudia kiasi cha Dola za Marekani 5,700 katika noti za Dola 100 ndani ya jeneza pale lilipofunuliwa.

Pesa hizo zilitolewa na kuwekwa kwa kiongozi wa Ukoo wa Okabo, Okii.

Kwa mujibu wa Ngole kaka yake alikuwa akipokea mshahara wa shilingi milioni 3 kwa mwezi huku mke wake akifanya kazi katika uwanja wa ndege wa Entebbe kama Afisa Mwandamizi wa Uhamiaji.

Akizungumza na mtandao wa hivisasa kwa njia ya simu kiongozi mmoja wa dini ameweka wazi kuwa hakuna kiasi chochote cha pesa duniani kinachoweza kutumika kama hongo kwa Mungu kwakuwa Mwenyezi Mungu hapokei kitu chochote kutoka kwa mwanadamu isipokuwa kufuata yale tu aliyoyaelekeza na yanayompendeza basi.

“Ni ujinga sana kumfananisha Mungu na mwanadamu ambaye anaweza akapokea kitu chochote na kufanya kinyume ikiwa kama rushwa, lakini kwa Mungu hakuna suala kama hilo. Njia pekee ya kuuona ufalme wa Mungu na kuepuka moto wa milele ni kupitia matendo mazuri yampendezayo Mungu,” ameongeza.

Amedai kuwa kwa Mwenyezi Mungu hakuna upendeleo wa aliyenacho au asiyekuwa nacho na kama mtu anataka msamaha wa dhambi zake ni bora kufanya hivyo angali bado akiwa hai kwa kutubu na kumrudia Muumba na sio kutegemea siku ya hukumu.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni