Habari/News

Ajali ya Jahazi yaua watu 12 na kujeruhi 33, Magufuli aomboleza

Tarehe January 11, 2017

screen-shot-2014-03-13-at-10-13-49-pm

Ajali ya  kuzama jahazi namba Z5512 MV Burudani iliyotokea usiku wa kuamkia jana na imesababisha vifo vya zaidi ya watu 12 na majeruhi zaidi ya 33.
Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia  tarehe 10 Januari, 2017 katika kisiwa cha Jambe  kilichopo katika bahari ya Hindi umbali mfupi kutoka Tanga Mjini, ambapo pamoja na vifo vya watu hao watu wengine 33 wamenusurika na 25 kati yao wamelazwa katika Hospitali ya Bombo Mkoani Tanga.

Kwa mujibu wa mmoja wa Manusura ameeleza kuwa chombo hicho kilipigwa na upepo mkali baharini na kukosa mwelekeo kisha kukatika vipande vipande.

“Baada ya kuondoka bandarini nahodha pamoja na wasaidizi wake walilazimika kusimamisha chombo kwa takribani saa mbili hivi ili kupisha upepo na baadaye tukaondoka, lakini hatukufika mbali chombo kikapigwa na wimbi na kupoteza mwelekeo ambapo baadaye kikajaa maji na kukatika katikati, “ alisema Emmanuel Mniga, mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, mkazi wa mkoa wa Morogoro, ambaye amelazwa katika wodi ya A1 katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo, Tanga.

Katika ajali hiyo, miili zaidi ya 12 ya baadhi ya abiria waliokufa maji katika jahazi hilo maarufu kwa jina la Sayari, lililokuwa likisafiri kutoka jijini Tanga kwenda mkoa wa Kaskazini Pemba, iliopolewa na imehifadhiwa katika chumba cha maiti cha hospitali hiyo ya Bombo.

Aidha abiria wengine zaidi ya 33 waliojeruhiwa, wamelazwa katika hospitali hiyo, ambapo wawili kati yao wanaendelea na matibabu chini ya uangalizi maalumu. Kati ya majeruhi hao, wamo watu wazima sita (6) na watoto sita (6) waliokuwa wakisafiri pamoja na wazazi wao katika chombo hicho, ambacho mpaka jana mchana idadi kamili ya abiria waliokuwemo haijafahamika.

Ilielezwa kuwa baadhi ya wakazi walioliona jahazi hilo kabla ya kuanza safari, walidai lilikuwa limebeba shehena ya mzigo ambao ni bidhaa mbalimbali ikiwemo pumba, maharage, vinywaji aina ya bia na abiria zaidi ya 50 wakiwemo watu wazima pamoja na watoto.

Kwa upande wake  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba alithibitisha tukio hilo na kusema walipokea taarifa za kupatikana kwa miili ya baadhi ya abiria hao jana saa 12.30 asubuhi na kuanza kufuatilia.

“Ajali ilitokea saa 7.30 usiku wa kuamkia jana na taarifa za awali zinaonesha chanzo cha ajali hiyo ni dhoruba kali,” alisema.

Aliongeza, “Tulipata taarifa ya kuzama majini kwa chombo hicho cha mv Burudani maarufu kama Sayari kinachomilikiwa na mkazi mmoja wa Pemba aliyetambulika kwa jina moja la Suleiman maarufu Bwimbwi….. Chombo hicho kilitokea bandari isiyo rasmi (bubu) eneo la Sahare hapa jijini Tanga kuelekea Kaskazini Pemba na ndipo kikakutwa na ajali hiyo, “ alisema.

Aidha, Rais Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na pia amewataka wote walioguswa na vifo hivyo kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki cha huzuni ya kuondokewa na jamaa zao.

Dkt. Magufuli pia amewatakia matibabu mema majeruhi wote walionusurika katika ajali hiyo ili wapone haraka, warejee katika familia zao na waendelee na ujenzi wa Taifa.

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni