Afya

Waziri wa Afya atema cheche Mgonjwa kupasuliwa Ubongo Kimakosa

Tarehe March 3, 2018

Waziri wa afya Sicily Kariuki nchini Kenya ametangaza kumsimamisha kazi Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Kenyatta nchini Kenya Lilly Koros kufuatia mgonjwa kufanyiwa upasuaji wa Ubongo kimakosa.

Mkasa huo  ambao umewashangaza wengi  umetokea katika hospitali hiyo wiki iliyopita na leo ilikuwa tarehe ya mwisho kwa maafisa wa matibabu ambao walihusika kueleza ilikuwaje hadi kosa hilo likatokea.

Taarifa ya Bi Koros iliyotolewa Alhamisi ilisema maafisa wanne wa matibabu walikuwa wamesimamishwa kazi, akiwemo msimamizi wa sajili ya watu wanaofanyiwa upasuaji wa ubongo.

Wengine ni mwuguzi aliyekuwa akisimamia wadi, mwuguzi wa kuwapokea wagonjwa kwenye chumba cha kufanyiwa upasuaji na afisa wa kuwatia ganzi wagonjwa.

Bi Koros alisema kupitia taarifa kwamba kosa hilo lilitokea pale mkanganyiko ulipotokea kuhusu wagonjwa wawili waliokuwa hawajitambui.

Mmoja kati yao ndiye alihitaji upasuaji wa kichwa ili kuondoa damu iliyokuwa imeganda kwenye ubongo wake.

Huyo mwingine alikuwa amefurwa kwenye kichwa lakini alihitaji matibabu ambayo hayakushirikisha upasuaji.

Lakini asiyehitaji upasuaji ndiye aliyeishia kufanyiwa upasuaji. Madaktari waligundua kosa hilo saa chache baada yao kuanza upasuaji walipogundua kwamba hawakuweza kuiona damu iliyoganda kwenye ubongo wa mgonjwa waliokuwa wanamfanyia upasuaji.

Bi Koros ameomba radhi na kusema “tunafurahi kuwatangazia umma kwamba mgonjwa huyo sasa ametibiwa na anaenedelea vizuri kupata nafuu”.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni