Afya

Jinsi unavyoweza kutibu magonjwa 10 kwa kula bamia

Tarehe February 2, 2018

 

MMEA wa bamia uzaao matuda yanayoliwa, ni zao linalostawi karibu maeneo yote hapa nchini, ingawa hustawi na hupendwa zaidi na watu wa ukanda wa Pwani. Huliwa kama mboga kwa matunda hayo kupikwa yakichanganywa na aina nyingine ya mboga kama vile nyama.

Watu wa ukanda wa Pwani hutumia bamia kwa kuikatakata vipande vidogo na kuchanganya vipande hivyo na  majani ya maboga, magadi kisha kupika pamoja na kupata mboga iitwayo mlenda au hombwe kwa watu wa pwani ya mkoa wa Tanga.

Kwa bahati mbaya sana walaji wengi hawajui umuhimu wake kiafya kama anavyobainisha Mtaalamu na Mkufunzi wa Chuo cha Tiba na Uuguzi ( IMTU) cha jijini Dar es salaam, Dk. Daniel Elifariji Mtango.

Mtaalamu huyo wa kitengo cha Afya na Jamii Chuoni hapo, anasema tunda la bamia lina vitamini A na B ambavyo huimarisha macho kutokana na  virutubisho hivyo kusheheni kiasi kingi cha protini ukilinganisha na lishe nyingine inayotokana na mimea.

Kama hiyo haitoshi, viini lishe vilivyomo husaidia kuwaokoa watoto wenye  tatizo la utapiamlo, vilevile huweza kuwaondoa watu katika hatari ya ugonjwa wa kisukari kwa  kuuweka sawa mfumo wa sukari mwilini.

Zinapoliwa kwa usahihi, huongeza kinga za mwili kwa watoto na watu ambao kinga yao ya mwili imeshuka na kuwa kwenye hatari ya kuambukizwa Virusi vya Ukimwi na magonjwa mengine yanayosababishwa na kushuka kwa kinga ya mwili, anasema.

Akifafanua zaidi, Dk. Mtango anasema, maji ya bamia husaidia kuzuia magonjwa ya moyo kwa kuifanya mishipa ya damu kufanya kazi vizuri kutokana na maji yake kuwa na uwezo  wa kuondoa lehemu kwenye kuta za mishipa ya damu.

“Lehemu zisipoondolewa kwenye mishipa hiyo husababisha msukumo wa damu kwenda vibaya na kuwa chanzo cha maradhi ya shinikizo la damu. Kwa hiyo tunaona ni kwa jinsi gani ambavyo mmea huu ulivyo muhimu katika lishe na kudhibiti magonjwa ambayo wakati mwingine hayawezi kutibiwa hapa nchini. Hivyo bamia inaweza kupunguza idadi ya watu kwenda India kutibiwa maradhi ya moyo,”anasema.

Faida zingine za ulaji wa bamia  ni kuzuia tatizo la watoto kupasuka uti wa mgongo au mgongo wazi, kumsaidia mama mjamzito pamoja na mtoto  tumboni  kuwa na afya  kabla na baada ya kujifungua.

Hutibu tatizo la kuchoka bila sababu, zaidi  kwa watu ambao wana msongo wa mawazo, ambao mtaalamu anashauri kundi hilo kula kwa wingi bamia kwani huleta matokeo ya haraka na kufanya afya zao kuimarika zaidi na kuwafanya  wawe na amani, furaha muda wote.

Faida nyingine; hutibu vidonda vya tumbo na kudhibiti bakteria wasababishao matatizo hayo na kupunguza uwezekano wa kupata saratani ya tumbo na huongeza kiwango cha uzalishaji wa damu kwa wingi mwilini.

Huimarisha nywele na kuzifanya ziwe na muonekano mzuri pamoja na kufanya utumbo mpana kubaki katika ulaini wa asili yake na kumkinga mtumiaji dhidi ya  saratani ya utumbo mpana (large intestine).

Pia hufanya mfumo wa usagaji wa chakula kuwa mzuri, na hivyo kupunguza maumivu makali wakati wa kwenda haja kubwa kutokana na majimaji ya bamia kulainisha choo kama ilivyo papai na ndizi mbivu. Pia huongeza hamu ya tendo la ndoa.

MATUMIZI:

  • Mlaji anaweza kupika bamia kama mboga kisha kuchanganya na chakula kingine na kula kama mlo. Vyakula hivyo vinaweza kuwa, uji, mchuzi, na vingine.
  • Matumizi mengine ni mtumiaji anatakiwa kukatakata bamia vipande vidogovidogo baada ya kuoshwa kwa maji safi na salama. Loweka kwenye maji kwa dakika kadhaa vipande hivyo kulingana na uwingi wa vipande vyenyewe ili kupata juisi.
  • Kunywa ujazo wa kikombe kimoja cha juisi ya bamia sawa na gramu 100. Au unaweza kula vipande hivyo vibichi vilivyojazwa kwenye kikombe cha ujazo huo.
  • Inashauriwa kuwa watoto wadogo wapatiwe zikiwa zimepikwa.  Fanya hatua hizo tatu kwa mfululizo na matokeo yake hujitokeza kuanzia juma la tatu au kabla.

Anatoa ushauri kwa wakulima kulima zao hilo kwa wingi kutokana na faida hizo za kiafya na kukifanya kilimo chao kuwa na tija. Ni zao linalokomaa kwa muda mfupi na hukabiliana na hali zote za hewa. Pia jamii kula kwa wingi bamia ili kupunguza matatizo ya kiafya ambayo baadhi yake ameyaanisha katika makala haya.

 

Email this page

To:
From
Subject
Message
Code

Maoni